Rum 2:1-11
Wewe
mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo
mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya
yale yale. Nasi twajua ya kuwa hukumu ya Mungu ni ya kweli juu yao wafanyao
hayo. Wewe binadamu, uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda yayo hayo
mwenyewe, je! Wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu? Au waudharau wingi
wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu
wakuvuta upate kutubu? Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na
toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya
haki ya Mungu, atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake; wale ambao kwa
saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika,
watapewa uzima wa milele; na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio
dhuluma, watapata hasira na ghad
habu; dhiki na shida juu ya kila nafsi ya
mwanadamu atendaye uovu, Myahudi kwanza na Myunani pia; bali utukufu na heshima
na amani kwa kila mtu atendaye mema, Myahudi kwanza na Myunani pia; kwa maana
hakuna upendeleo kwa Mungu.
Wimbo wa Katikati
Zab 62:1-2, 5-6, 8
Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya,
Wokovu wangu hutoka kwake.
Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu,
Ngome yangu, sitatikisika sana.
(K) Bwana humlipa kila mtu sawasawa na haki yake.
Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya.
Tumaini langu hutoka kwake.
Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu,
Ngome yangu, sitatikisika sana.
(K) Bwana humlipa kila mtu sawasawa na haki yake.
Enyi watu, mtumainini sikuzote,
Ifunueni mioyo yenu mbele zake;
Mungu ndiye kimbilio letu.
(K) Bwana humlipa kila mtu sawasawa na haki yake.
Somo la Injili
Lk 11:42-46
Yesu aliwaambia Mafarisayo: Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili. Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo. Mtu mmoja katika wana-sheria akajibu, akamwambia, Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi. Akasema, Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu.

Post a Comment