Mpako wa wagonjwa: kuomba kwa imani kutamponyesha mgonjwa.
"Mtu wa kwenu amekuwa hawezi?Na awaite wazee wa Kanisa ;nao wamwombee na kumpaka mafuta kwa jina la Kristu.Na kuomba kule kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule na Bwana atamwinua ;hata ikiwa amefanya dhambi,atasemehewa."(Yakobo 5:14-15).
Hivyo kanisa huiadhimisha sakramenti hii kwa waumini wanapokuwa wagonjwa. kwa bahati mbaya,wakristo wengi hawaelewi maana ya sakramenti hii .Huenda waiona kama tangazo rasmi kwamba mtu anakaribia kifo na huogopa! Kudanganyika huko huleta hasara.
Mambo muhimu yapatikanayo katika sakramenti ya mpako wa wagonjwa.
1.Hutia nguvu kwa utu mzima. Katika sakramenti hii ,neema ya pekee ni Roho mtakatifu inayoleta msaada kwa mgonjwa kwa wokovu wa utu wake mzima.Imani yake kwa Mungu huinuliwa,na anathibitishwa kwa vishawishi na hofu vinavyoletwa na mawazo ya ugonjwa mbaya na kifo.Neema hiyo inampa amani ya roho.na kama Mungu anapenda ,yaweza hata kumponyesha kabisa mgonjwa na tena humletea maondoleo ya dhambi zake.
2.Kuomba kwa imani.
Mpako wa wagonjwa unayo ndani yake sala ya imani .Ni sakramenti ya imani kama sakramenti zingine.Imani hii ni jambo la maana kwa wote wawili;kwa yule anayetoa sakramenti na kwa yule anayeipokea na pia kwa wote wamwombeao mgonjwa.
3.Kupaka mafuta
Sala ya kubariki mafuta hueleza vizuri maana ya mafuta,ikidhihirisha matumaini na imani ya wote wanaohusika:
"Mungu Baba wa faraja yote, ilikuwa mapenzi yako kwamba wagonjwa ,katika udhaifu wao ,waponyeshwe na mwanao,sikiliza sala ya imani ,Umtume Roho mtakatifu kutoka juu ...juu ya mafuta haya yanayotolewa na mzeituni ...kwa kuponya mwili. Kwa baraka yako ,yawe chemichemi ya nguvu kwa mwili ,akili na roho ya wote wanaopakwa nayo .Yaondoe maumivu ,udhaifu na maradhi yote."
Wajibu wetu kama wakristu.
Kama wakristu tunapaswa tutambue hali ya mgonjwa ,tukijitahidi kumpa moyo kwa kumtunza vema na kuangalia mahitaji yake,kimwili(dawa,vyakula,raha,.....) na kiroho (sala na sakramenti). Na pia tusiitambue sakramenti hii ya mpako wa wagonjwa kuwa sakramenti ya wanaokaribia kufa;bali mtu akipata ugonjwa mkubwa,tusichelewe kumwita padre au katekista ,atakayeweza kuja kuongoza sala ,tukikumbuka ya kuwa kuomba kwa imani kutamponyesha mgonjwa ,kama ni mapenzi ya Mungu....Atakalo lifanyike...

Post a Comment