EKARISTI
TAKATIFU
Ekaristi Takatifu
ni Sakramenti ya Mwili na damu ya Yesu Kristo, ulio kweli katika Maumbo ya
mkate na Divai. Ni fumbo la ukombozi wetu aliloweka kristo siku ya Alhamisi Kuu
katika karamu ya mwisho alipoketi kuumega mkate pamoja na wanafunzi wake. Ambapo
fumbo hili liliweza kukamilika baada ya Kristo kujitoa sadaka msalabani kwa
ajili ya dhambi zetu.
Je, Fumbo Hili la Ekaristi Takatifu,
hukamilika wakati gani?
Kama vile Kristo alivoweza kuanzisha Sakramenti
hii kwa kuumega mkate na kuikamilisha
katika mlima kalvari (Golgotha), nasi tunaaswa katika ulimwengu wa sasa,
kwamba baada ya kuupokea Mwili na damu ya bwana wetu Yesu kristo kupitia
maadhimisho ya Misa Takatifu, tunampokea Kristo ndani ya mioyo yetu na kupitia
Neema za sakramenti hii, Kristo anaishi ndani yetu nasi ndani yake. Hivo,
tunaaswa kwenda kuuishi ukristo wetu katika mazingira na maisha yetu ya kila
siku, ili huyu Kristo tuliyekubali kumpokea aishi ndani yetu na ajidhihirishe
kupitia matendo yetu mema yanayomtukuza Mwenyezi Mungu, kama vile kuwagusa
wahitaji na kuuishi upendo kwa ndugu zetu.
Je, fumbo la Ekaristi Takatifu limetajwa wapi katika agano la
kale?.
Ekaristi Takatifu imeweza kuelezewa na kufananishwa na Mana
iliyoshuka kutoka mbinguni kwa wana wa Israeli walipokua jangwani baada ya kumnung'unikia Mwenyezi Mungu kupitia mtumishi wao Musa.
(Kut 16:4) “ndipo bwana akamwambia Musa,
tazama mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu
watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba
watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo.” Tunaona Mungu anawashibisha wana wa Israeli chakula
kutoka mbinguni (Mana) ambamo kupitia chakula hicho, jina lake liweze kutukuzwa, Vivyo
hivo hata sasa Mwenyezi Mungu anatulisha mwili na damu ya mwanae kupitia Mafumbo
ya Ekaristi Takatifu ili kupitia huo naye kukaa kwetu, tupate neema za kuishi
kwa kadri ya sheria yake.
Vilevile imeandikwa; (kut 16:16-18) "Neno hili ndilo aliloagiza Bwana, Okoteni
ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi, kama hesabu ya
watu wenu ilivyo; ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani
mwake. Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine
kupungua. Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa
na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu
kama ulaji wake ulivyokuwa."
Hivo kupitia mstari tajwa hapo juu, Kristo anajihirisha katika Ekaristi Takatifu
ya agano jipya ambapo kama wakristo wakatoliki, apokeae Ekaristi nusu (kiumbo)
na yule aliyepokea mkate mzima wote ni sawa na wanampokea Kristo aliye kamili
katika roho zao wala hakuna anayepungukiwa, wala kuzidishiwa.
Fumbo la Ekaristi
Takatifu katika Agano jipya.
Fumbo hili la mwili na damu ya Bwana wetu Yesu
Kristo, katika agano jipya linadhihirishwa kwanza katika karamu ya Mwisho siku
ya Alhamisi kuu Kristo alipoketi na mitume wake kuumega mkate,
Turejee; (Lk 22:19-20) “Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili
wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe
nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika
damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.].”
Vilevile katika barua ya Mtume Paulo (1 Kor 11:23-26) “Kwa
maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule
aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio
mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi
hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya
katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila
mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata
ajapo.”
Je, Ekaristi Takatifu ina nguvu au umuhimu
gani kwa mkristo?
(Gal 2:20) “Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni
hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa
katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa
nafsi yake kwa ajili yangu”. Basi wakristo wenzangu, tuulapo mwili wa Kristo na kukinywea
kikombe chake si sisi tena tunaojiongoza bali ni kristo ndiye aishiye ndani
yetu.
Hivo Kristo
anatulisha mwili wake katika Ekaristi Takatifu ili kwa imani tubadilishwe kutoka katika
madhaifu yetu na kupokea umungu wake na ustahimilivu katika kuyashika
maagizo yake na kuiepuka dhambi. Mfano; Ni wazi kwamba, kwa hali ya kawaida na katika madhaifu
ya ubinadamu wetu yaweza kuwa ngumu sana kumsamehe jirani yako aliyekukosea. Lakini kwa nguvu ya Kristo yote yawezekana, yaani twaweza kusamehe
kwa wepesi na kusahau kwani si sisi tena tunaotenda kazi peke yetu, bali ni Kristo
anayeishi ndani yetu ndiye aitendaye kazi yake. Kumbe basi, twaweza kuepuka hatari ya
dhambi zote katika yeye atutiaye nguvu, rejea; (Flp 4:13) “Nayaweza mambo yote katika
yeye anitiaye nguvu.”
Je, twapaswa kupokea Ekaristi Takatifu tukiwa
katika hali gani?
Twapaswa kupokea mwili na damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwanza tukiwa na neema ya utakaso, yaani tusiwe na dhambi ya Mauti (Dhambi tunazozifanya kwa makusudi, kwa
kujiambua, na kwa hiari, kwani tunaamua kwa akili zetu kuyafanya mapenzi
yetu na kuyapuuza mapenzi ya Mwenyezi Mungu, hivo tunajitenga kabisa na upendo wa Mungu na kukosa ushirika naye.)
Pili, kwa kuungama
dhambi nyepesi kila mara tunapoanguka, (kuhusu
dhambi kubwa na dhambi nyepesi rejea, 1 Yoh 5:16-17). Tatu tunaaswa kufunga
kabla ya adhimisho la Misa Takatifu ili kuandaa roho zetu kumpokea Kristo kwani
yeye ndiye uzima wetu na tumaini letu na Nne twapaswa kumtambua, kumwamini na
kumkiri Kristo aliye kweli katika maumbo ya mkate na divai kuwa ndiye mwokozi
wa maisha yetu na muweza wa yote atupatiaye nguvu ya kuyashinda majaribu yote.
Je, kuna Madhara gani ya kupokea Ekaristi Takatifu,
isivyostahili?.
Imeandikwa; (1 Kor 11:27-32) “Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea
kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na
damu ya Bwana. Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea
kikombe. Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa
kutokuupambanua ule mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na
dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi
zetu, tusingehukumiwa. Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa
adhabu pamoja na dunia.”
Hivyo, wakristo wenzangu, tunapopokea
Ekaristi Takatifu isivyotahili (kama vile kuwa na dhambi ya mauti, kutokuwa na
uelewa kamili wa kile tunachoenda kukipokea na kupokea kwa mazoea) au katika
hali isiyo ya utakatifu, kwanza ni kufuru juu ya Sakramenti, na pili twaupokea mwili na damu yake Bwana wetu Yesu Kristo
lakini sio neema zake. Hivo tunakosa neema ya Kristo kujidhihirisha katika
maisha yetu na matendo yetu.
Shetani huendelea kufanya kazi katika maisha yetu
kama ilivyokuwa awali tukiwa wadhambi na kabla ya kupokea nguvu ya Kristo kupitia Sakramenti ya Ekaristi
Takatifu. tunaona ambavyo Yuda mwana wa Iskariote alivyoshindwa kukiri makosa yake
mbele ya Kristo na maamuzi yake ya kumsaliti Kristo kabla ya karamu ya mwisho,
naye alipopokea mkate shetani alimwingia na akaendelea kufanya kile alichokipanga bila ya kufaidika chochote kwani alimpokea Kristo lakini sio
neema zake kulingana na dhambi alokuwa nayo. Turejee (Yn 13:26-27) “Basi Yesu
akajibu, Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge,
akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Na baada ya hilo tonge
Shetani alimwingia. Basi Yesu akamwa mbia, uyatendayo yatende upesi.”
Hitimisho.
Ekaristi Takatifu
ni fumbo linalonoa uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu, linaimarisha roho zetu na
hamu ya kuendelea kumtafuta yeye, hivo kama wakristo wabatizwa na tuliopokea
Sakramenti ya Komunyo twapaswa Kupokea Ekaristi Takatifu mara kwa mara katika hali ya
utakatifu na tafakari ili zile neema zinazopatikana kupitia kuupokea mwili na
damu wa Bwana wetu Yesu Kristo zitusaidie kuyabadili maisha yetu kutoka ukale
usiofaa na tuweze kuyaishi mafundisho yake kwa Imani na matendo.
Tukumbuke kwamba, tunayotenda dhambi tunapoteza uhusiano wetu na Mungu, ambapo bila Baba hakuna Mwana, hivo tunakosa ushirika tena na Kristo kwa kumkaribia shetani na maovu yake, hivo tuzidi kuimarisha uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu kwa kufanya Toba kila tunapoanguka, tudumu katika njia njema na tuzidi kujiimarisha kupitia nguvu ya Kristo kupitia fumbo la Ekaristi Takatifu.
Basi, Tumwombe Mwenyezi Mungu atuongezee imani juu ya Fumbo hili la Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu kristo, Mungu-mtu katika maumbo ya mkate na Divai, na imani hiyo itujapatie nguvu za kuuishi ukristo wetu na mapendo kwa jirani zetu katika mazingira na maisha yetu ya kila siku mwisho tufike kwake juu mbinguni.
Tumsifu Yesu kristo...

Post a Comment