SALA
Sala ni kuinua mioyo yetu kwa Mungu na kuongea nae. Hivo sala sio kuongea tuu, bali ni kuongea na kusikiliza. Mungu anatualika tuongee nae kwa kusema na kusikiliza. Katika maandiko matakatifu tunakumbushwa; “Niite, nami nitakujibu na kukuambia mambo makubwa yaliyofichika ambayo hujapata kuyajua” (Yeremia 33:3)
Hivo basi vile tunavyokuwa na juhudi ya kusali kwa kusema mbele ya Mungu ndivyo vivyo hivyo tunatakiwa tuwe na juhudi ya kumsikiliza Mungu kile anachotuambia. Tunaweza kumsikiliza Mungu ndani kabisa ya Mioyo yetu, mara nyingine kwa kupitia dhamira zetu, kupitia watu wengine na kupitia neno lake (Biblia). Basi Tuombe neema ya kutambua sauti yake anaposema nasi ili tuweze kumsikiliza na kutengeneza mahusiano mazuri kati yetu na yeye.
Mungu ni Baba yetu, anatupenda sana na yupo tayari kutusikiliza wakati wote, ndio maana Mungu anatualika kwa kutuambia; “Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”. (Isaya 1:18). Tudumu katika sala daima kwa sababu njia ya sala ndipo tunaweza kusema yale tunayotaka mbele ya Mungu na kusikia yale anayotaka Mungu.
Je, kwanini huwa tunasali?
Tunasali ili kudumisha mahusiano yetu na Mungu na ili kutimiza wajibu wetu Mbele ya Mungu. Hivo zipo Sababu kuu za kusali nazo ni; Kumwabudu Mungu, Kumshukuru Mungu, Kuomba neema na baraka kwa ajili yetu na wenzetu, Kuomba msamaha, Kumsifu na kumtukuza Mungu
1. Kumwabudu Mungu
Tunasali ili kumwabudu Mungu, yaani kumpa heshima ya mwisho juu ya kila kitu. Kuonyesha kuwa ni mkuu na wa kipekee kuliko mtu au kitu chochote.
2. Kumshukuru Mungu
Pia tunasali ili kumshukuru Mungu kwa yale yote aliyokwisha kuyatenda, anayoyatenda na yale atakayoyatenda. Tunamshukuru Mungu kwa yote kwa kuwa yote anayoyafanya anayafanya kwa Mapenzi/ Matakwa yake Matakatifu. Nia ya Mungu ni njema daima ndio maana tunapoona ameruhusu mambo ambayo kwa akili zetu tunayaona ni magumu na sio mema tunapaswa kushukuru kwa sababu ameyafanya kwa makusudi mema.
“Furahini siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu” (1 Wathesalonike 5:16-18). Hivo Tunatakiwa kumshukuru Mungu kwa Kila jambo na kumshukuru huku ni kwa njia ya sala.
3. Kuomba neema na baraka kwa ajili yetu na wenzetu
Tunasali kwa kuomba neema na baraka kwa ajili yetu sisi wenyewe na kwa ajili ya wenzetu. Tunamuomba Mungu baraka na Mkono wake katika yale tunayoyafanya na kwa yale wanayoyafanya wengine. Maombi yetu ili yakubalike mbele ya Mungu ni lazima yawe katika mapenzi yake na yawe na nia njema. Tunambushwa katika biblia; “Tena, mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya; mnaomba ili mpate kutosheleza tamaa zenu.” (Yakobo 4:3) Hivo basi twapaswa kusali kwa kuomba mema na kwa nia njema ili tuweze kupata yale tunayoyaomba kwa Mungu.
4. Kuomba Msamaha
Tunasali ili kuomba msamaha mbele ya Mungu kwa yote mabaya tuliyoyafanya. Mungu ni mwaminifu hasa kwenye kutusamehe na kutuondolea dhambi zetu. “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” (1 Yohana 1:9)
Vilevile Tunatakiwa kusali katika mapungufu yetu na kuwa na matumaini. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; “maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu”. (2 Wakorinto 12:9)
5. Kumsifu na kumtukuza Mungu
Tunasali ili kusifu na kumtukuza Mungu. Mungu anapenda kusifiwa na kutukuzwa. Kwa njia ya sifa tunapokea neema na baraka hata ambazo hatujaziomba. (Zaburi 100:1-4)
Je, kama wakristo Yatupasa kusali lini?
Yatupasa kusali kila siku bila kukata tamaa (Lk 18:1) Sala ndiyo njia pekee ya kutuunganisha na Mungu. Tunatakiwa tusali daima Kama Yesu alivyotuhimiza kwa mfano huu; (Lk 18:1-8)
Hivyo basi, Tunapaswa kusali daima kila siku, kila saa na katika hali yoyote. Tusichoke kusali hata kama maombi Yetu hayajajibiwa. Mungu ni mwenye Hekima na anajua lini hasa akujibu kile unachokiomba kwa manufaa yako wewe. Usipopewa Leo kile ukiombacho unaweza kukipata kwa wakati ufaao tena bila ya Kukiomba, na tukumbuke kuwa Sala ni hazina, kwani sala unayosali leo inaweza kukunufaisha wakati usioutarajia.
Je, nini maana hasa ya Sala kwa Mkristo Mkatoliki?
Maana ya sala kwa Mristu Mkatoliki sio kuomba tuu. Sala kwa Mkatoliki ni zaidi ya kuomba. Kwa Mkatoliki sala inamaanisha kufanya haya; Tunasali kushukuru, Tunasali kuomba, Tunasali kusifu na Kutukuza, Tunasali kumshirikisha Mungu Furaha zetu na huzuni zetu, Tunasali kuomba Toba na Msamaha, Tunasali kumshirikisha Mungu Juhudi zetu na Mipango yetu, Tunasali kumshirikisha Mungu changamoto zetu.
Hivo tuna kila sababu ya Kusali kila Siku na Kila saa. Maisha yetu yote yanatakiwa yawe Maisha ya Sala. tusifikiri kwamba Wakati wote tunaposali lazima tutamke maneno Mengi sana ili tuwe tumesali, Sala haipimwi kwa Maneno, bali Sala hupimwa kwa nia yake na Kujiweka wazi mbele ya Mungu.
Basi kila Usalipo Jijengee Tabia ya kunuia, kuwa wazi na kusali kwa ukweli wa Moyo wako. Hata kama ni sentesi Moja fupi Kabisa itamke kwa Upendo na Imani. Kwa Mfano; kuna wakati inatosha kabisa kusema Ee Mungu wangu ninakushukuru kwa hili. hii inaweza kuwa sala Yenye nguvu Kama imetamkwa kwa Imani, Shukrani na Mapendo ya Kweli. Maneno machache yanayotamkwa kwa Imani na Mapendo yanaweza kuzidi Mkesha wa Kusali Usiku Mzima huku unasinzia.
Lakini, pamoja na kwamba sala fupi ni nzuri na inafaa sana, kuna haja pia ya kujitengea Muda wa Kutosha Kusali na Kutafakari Huku tukiungana na Mungu. Kila siku tunanye mambo yote mengine lakini tusisahau kuwa Tunahitaji kuwa na Muda wa Kusali. Tusali daima, Kila wakati na Maisha yetu yawe ni Maisha ya Sala.
Je, Yatupasa kusali namna gani?
Yatupasa kusali kwa Unyenyekevu, Ibada, upendo, Matumaini na kwa Saburi. Yesu alitufundisha kuhusu kusali kwa kutumia mfano huu; “Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa”. Luka 18:9-14
Tunatakiwa tusali kwa nia njema na kwa kufuata Mapenzi ya Mungu ili sala zetu zipate kibali mbele za Mungu. Tunapoomba kwa nia mbaya ya tamaa na majivuno hatuwezi kupata kile tukiombacho. Rejea; (Yakobo 4:3) “Tena, mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya; mnaomba ili mpate kutosheleza tamaa zenu”. Hivo mpendwa, Kila unaposali jiulize unasali kwa kwa sababu gani? Kila ubapoomba, jiulize unamuomba Mungu ili nini? Sababu yako ndio kibali cha sala yako.
Waweza jiuliza, je, Sala zipo za namna ngapi?
Kutokana na mapokeo ya kanisa Katoliki, Sala zipo za namna tatu; Moja Sala ya Taamuli ambayo ni sala ya kumtazama tuu Mungu kwa upendo mkubwa moyoni. Pili Sala ya Sauti ambayo ni sala asaliyo mtu au kundi kwa kutamka maneno. Na tatu ipo Sala ya Fikra ambayo ni sala asaliyo mtu peke yake au akiwa na wengine kimya kimya akimuwaza Mungu.
Je, sala zetu zinaweza kuwaendea Watakatifu?
Ndiyo, sala inaweza kuwaendea Mama na marafiki wa Yesu (watakatifu), walioungana naye kuwa mwili mmoja, wasiweze kutenganishwa na chochote. Rejea; (Rom 8:38-39). “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu”. Pia rejea; (Flp 1:21, 23) “Kwangu mimi kuishi na Kristo, na kufa ni faida… Ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo”.
Kwa kuwa hao wako na Kristo mbinguni, wanatuombea mfululizo pamoja naye. “Niliona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao. Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, ‘Ee Mwenyezi, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini…” (Ufu 6:9-10). Hivo Tunawaomba wazidi kutuombea kwa Mungu, kama tunavyowaomba wenzetu waliopo duniani. “Mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; pia na kwa ajili yangu mimi” (Ef 6:18-19).
Je, sala inategemea maneno?
Hapana, sala haitegemei maneno mengi mazuri, bali kujijenga “juu ya imani… na kuomba katika Roho Mtakatifu” (Yud 20). Pia rejea; (Math 6:7) “Mkiwa katika kusali, msipayukepayuke, kama watu wa mataifa; maana hao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi” Hii haituzuii tusirudie maneno yetu kwa dhati zaidi na zaidi. “Yesu alikwenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yaleyale” (Math 26:44).
Lakini pia Tunaweza kusali kimoyomoyo, tunaona; “Hana alikuwa akinena moyoni mwake, midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe… ‘Nimeimimina roho yangu mbele za Bwana’” (1Sam 1:13,15). Pia rejea; (Zab 19:14). “Maneno ya kinywa changu, na mawazo ya moyo wangu, yapate kibali mbele zako, Ee Bwana”.
Je, Roho Mtakatifu anatusaidiaje kusali?
Roho Mtakatifu anatusaidia tusali kama Yesu, akiwa mlezi wa ndani na kutumia vipaji vyake saba. “Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!” rejea (Gal 4:6). “Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa… huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu” rejea (Rom 8:26-27). Ndiyo sababu Kanisa linatuhimiza tumtamani na kumualika kila mara, ‘Njoo, Roho Mtakatifu!’ yaani kumuomba Baba kwa njia ya Mwana amtume zaidi na zaidi ndani mwetu.
Tumsifu Yesu Kristo…
Post a Comment