SOMO 1: Rum 13:8-10

Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria. Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani, na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria.

WIMBO WA KATIKATI 

Zab.112:1-2, 4-5, 9

Aleluya.
Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendezwaye sana na maagizo yake.
Wazao wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
(K) Heri atendaye fadhili na kukopesha.
Nuru huwazukia wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki.
Heri atendaye fadhili na kukopesha;
Atengenezaye mambo yake kwa haki. (K)
Amekirimu, na kuwapa maskini,
Haki yake yakaa milele,
Pembe yake itakuzwa kwa utukufu. (K)

Shangilio

Mt 11:25

Aleluya, aleluya,
Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu nan chi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya.


INJILI: Lk 14:25-33

Makutano mengi walipokuwa wakifuatana na Yesu, aligeuka, akawaambia, Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume kwa wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali. Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

Neno la bwana..........

Post a Comment

Previous Post Next Post