Tumsifu Yesu kristu........


Katika mapito yetu ya imani, tunaendelea na safari kwenye bahari isiyotabirika ya maisha, tukikumbana na dhoruba za majaribu na mitihani inayotukosesha usingizi. Lakini hebu tusiwe na hofu, kwani tumeahidiwa, "Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu" (Isa 55:6). Kama vile dhahabu inavyochomwa katika moto ili kutoa uchafu na kuiweka safi, vivyo hivyo safari yetu ya imani inahitaji kukabiliana na changamoto ili tupate utakaso na kukua.



Tunapoomba na majibu hayaji mara moja, tunakumbushwa kwamba Mungu anaweza kuturuhusu kupitia magumu kama vile magonjwa, kufeli, madharau, vifo, na hata msongo wa mawazo. Hata hivyo, tusisahau ahadi yake inayosema, "Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho" (Yer 29:11). Kwa hiyo, tukiwa na subira na imani, tunaweza kutegemea kuwa kila hatua inaongozwa na mkono wa upendo.



Katika sala zetu na kutafakari Neno la Mungu, tunagundua nguvu katika maneno yake: "Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa" (Mt 7:7).


Hivyo kama mvua ishukavyo na theluji kutoka mbinguni, neno la Mungu linashuka kwetu kuleta uhai na kukua kwetu. "Neno langu litokalo katika kinywa changu halitarudi bure, bali litatimiza mapenzi yangu" (Isa 55:11). "Majibu ya maombi yetu yanaweza kuwa kama mchakato wa kukomaa, lakini ni katika subira hiyo tunapogundua utimilifu wa ahadi zake."




Yesu mwenyewe alipitia njia hii ya mateso, akajua uchungu wa kusema, "Mungu wangu, mbona umeniacha?" Lakini kwa imani, alibaki mwaminifu hadi mwisho na sasa Jina lake limetukuzwa kuliko yote. Kumbuka, ushindi ni wetu, na kwa kuvumilia, tunaweza kufurahia matunda ya ushindi.


Tusisahau kuwa Mungu anajua anachofanya, na kila jaribu linafanya kazi kwa wema wetu. "Kumbuka ni washindi tu hufurahia matunda kuwa mmoja wao." Dunia inaweza kuwa na kanuni zake, lakini neno la Mungu litatimiza mapenzi yake. Kwa hiyo, tusiwe na wasiwasi wakati majibu yanachelewa; badala yake, amini kuwa Mungu anatayarisha kitu cha kipekee kwa ajili yako.



HITIMISHO 

Katika safari hii ya imani, tusikate tamaa. "Twende pamoja tupendane naam tuwe pamoja." Kwa kushirikiana na wenzetu, tuwe chanzo cha faraja na mwanga. Tutumieni neno la Mungu  kuwahamasisha wale wanaohitaji nguvu na faraja. Mataji yetu ya ushindi yanatusubiri, na kila hatua ya safari inatufikisha karibu na ushindi huo.

AMANI NA SALAMA.....




Post a Comment

Previous Post Next Post