MASOMO YA MISA, AGOSTI 13, 2024
JUMANNE, JUMA LA 19 LA MWAKA
SOMO 1
Eze. 2:8 – 3:4
Ezekieli aliisikia sauti, ikamwambia: Mwanadamu, sikia neno hili ninalokuambia; usiwe wewe mwenye kuasi kama nyumba ile yenye kuasi; funua kinywa chako, ule nikupacho. Nami nilipotazama, mkono ulinyoshwa kunielekea; na tazama, gombo la chuo lilikuwa ndani yake. Akalikunjua mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole!
Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli. Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo. Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.
Akaniambia, Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli, ukawaambie maneno yangu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 119:14, 24, 72, 103, 111, 131 (K) 103
(K) Mausi yako ni matamu sana kwangu.
Nimeifurahia njia ya shuhuda zako,
Kana kwamba ni mali mengi.
Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu,
Na washauri wangu. (K)
Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
Mausia yako ni matamu sana kwangu,
Kupita asali kinywani mwangu. (K)
Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele,
Maana ndizo changamko la moyo wangu.
Nalifunua kinywa changu nikakweta,
Maana naliyatamani maagizo yako. (K)
SHANGILIO
Yn. 17:17
Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya.
INJILI
Mt. 18:1 – 5, 10 , 12, 14
Wanafunzi walimwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
Basi, yeyote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.
Na yeyote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi.
Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika zao mbinguni sikuzote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni.
Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi wale tisa na tisini, akaenda milimani, na kumtafuta yule aliyepotea? Vivyo hivyo haipendezwi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Post a Comment