Somo la Kwanza
Mdo 25:13-21
Siku zile, Agripa mfalme na Bernike walifika Kiaisaria,
wakimwamkia Festo. Na walipokuwa wakikaa huko siku nyingi, Festo akamweleza
mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki
kifungoni; ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi
wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake. Nikawajibu kwamba si
desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa
hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika
mashitaka yake. Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi
katika kiti cha hukumu nikaamuru mtu huyo aletwe. Na wale waliomshitaki
waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama nilivyodhani, bali walikuwa na
maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika habari ya
mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema kwamba yu
hai. Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza
kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya. Lakini Paulo
alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru alindwe hata nitakapompeleka
kwa Kaisari.
Neno la Bwana, Tumshukuru Mungu.
Wimbo wa Katikati
Zab 103:1-2, 11-12, 19-20
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni.
Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
(K) Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni.
Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni,
Na ufalmc wake unavitawala vitu vyote.
Mhimidini Bwana, enyi malaika zake,
Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake,
Mkiisikiliza sauti ya neno lake.
(K) Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni.
Shangilio
Kol 3:1
Aleluya, aleluya,
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu,
Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
Aleluya.
Somo la Injili
Yn 21:15-19
Walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni
wa Yohane, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa
nakupenda. Akamwambia, Lisha wanakondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili.
Simoni na Yohane wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa
nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa
Yohane, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu,
Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa
nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu. Akasema, Amin, amin, nakuambia,
Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini
utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua
usikotaka. Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza
Mungu. Naye akiisha kusema hayo, akamwambia, Nifuate.
Post a Comment