LEO JULAI 22, TUNAYAKUMBUKA MAISHA YA MTAKATIFU MARIA MAGDALENA (KARNE YA KWANZA).
Maria Magdalena alikuwa mzaliwa wa kikiji kiitwacho Magdala karibu na ziwa Galilaya (Israeli).
Katika miaka ya nyuma aghalabu huyu hakutofautishwa barabara na yule mwanamke mkosefu ambaye machozi yake yalimdondokea Yesu miguuni mle nyumbani mwa Simoni Mfarisayo.
Katika Injili ya Luka (8:1-3) imeandikwa hivi: "Yesu alipopitia katika miji na vijiji akitangaza habari njema ya Utawala wa Mungu, wale kumi na wawili waliandamana naye.
Pia wanawake kadhaa waliokuwa wamepandwa na pepo waliandamana naye.
Kati yao Maria aitwaye Magdalena ambaye alitolewa pepo wabaya saba."
Hatusemi ya kwamba kwa sababu mtu alikuwa amepagawa na pepo wabaya kwa hiyo alikuwa mtu mbaya au mkosefu.
Huenda wale pepo saba ndio waliosababisha awe mgonjwa sana Kama vile wale wengine waliokuwa wamepandwa na alimponya kwa kuwafukuza wale pepo.
Kwa vyovyote vile Injili haitoi habari ya kwamba Maria Magdalena alikuwa mkosefu na mwasherati bali tunajua kwa hakika kwamba alikuwa mmojawapo wa akina mama wema na hodari waliofuatana na Yesu katika safari zake za kitume na kumuhudumia Bwana kwa mali yao.
Alikuwa na upendo mkubwa sana kwa Bwana Yesu nao unadhihirishwa wazi sana katika Injili.
Wakati wa mateso ya Yesu, Bikira Maria pamoja na Maria Magdalena na Mtume Yohane walisimama karibu na Msalaba alipozimia Roho na alisaidia kuushusha mwili wa Yesu na kuuzika.
Yesu alipofufuka Jumapili asubuhi na mapema, alijionyesha kwanza kwa Maria Magdalena.
Hivyo ndivyo alivyoandika mwinjili Marko.
Na mwinjili Yohane ameandika kwamba mama huyu alikuwa analia kwa uchungu sana kwa kuwa alidhani mwili wa Bwana wake mpendwa ulikuwa umechukuliwa.
Mara Yesu alimtokea akamwambia aende kuwapasha habari Mtume kwamba yeye amefufuka kweli kama alivyowahi kusema.
Japo kuna hadithi nyingi juu ya maisha yake ya baadaye hizo haziwezi kuthibitishwa.
MTAKATIFU MARIA MAGDALENA, UTUOMBEE.
Post a Comment