KILA MWAKA AGOSTI 29 MAMA KANISA ANAFANYA KUMBUKUMBU YA KUKATWA KICHWA KWA YOHANI MBATIZAJI

Kukatwa kichwa kwa Yohane Mbatizaji kulikuwa hivi:

Zamani za Bwana wetu Yesu Kristo, Herode Mfalme wa Galilaya alitoa amri ya kumkamata Yohani Mbatizaji, na kumfunga gerezani kwa shauri la Herodia. 

Sababu ya kutoa amri hiyo ni kwamba Yohani hakuogopa kumkaripia Herode na kumwambia: "Huna ruhusa kukaa na mke wa ndugu yako" Mwanamke huyo ndiye Herodia. Lakini Herode hakuthubutu kumwua kwa kuwa Yohani Mbatizaji aliheshimiwa na watu wote kwa ajili ya Utakatifu wake.

Basi, kwa kuitukuza sikukuu ya kuzaliwa kwake, Herode aliwafanyia karamu wazee wa ikulu. Salome, binti wa Herodia aliingia chumbani walimokaa akaanza kucheza ngoma mbele yao. 

Herode akapendezwa sana pamoja na wazee wote waliokuwamo humo chumbani; akaapa kwa kiapo kumpa kitu chochote atakachotaka Salome hata kama ni nusu ya ufalme wake.

Msichana alitoka akamwambia mama yake: "Nitaomba nini?" Herodia akamwambia: "Kichwa cha Yohani Mbatizaji". Akarudi haraka mezani akanena: "Unipe sasa hivi katika sahani hili kichwa cha Yohani Mbatizaji". 

Mfalme akasikitika rohoni lakini kwa sababu alikuwa ameapa mbele ya wageni wake, aliogopa kukataa. 

Akatuma mmoja wa askari zake kumkata kichwa Yohani Mbatizaji. Askari akafanya vile na kuleta kichwa cha Yohani katika sahani.

Wakaja wafuasi wa Yohani Mbatizaji, wakauzika mwili wa shahidi Mtakatifu huyu kwa heshima.

Hatimaye Mungu aliwaadhibu Herode na Herodia. Waroma waliwahamishia Ufaransa na hapo ndipo walipofariki dunia mbali na nchi yao wenyewe.


MTAKATIFU YOHANE MBATIZAJI, UTUOMBEE..

Post a Comment

Previous Post Next Post