MTAKATIFU KLARA WA ASIZI (1253)

MTAWA NA MWANZILISHI WA SHIRIKA.

Leo Agosti 11, tunayakumbuka maisha ya Mtakatifu Klara wa Asizi. 

Klara alizaliwa Asizi mwaka 1194 hivi, zamani ya Mtakatifu Fransisko.  Tangu utoto wake alipenda zaidi kukaa katika upweke akiisali na kufunga. Badaye aliona  mwenendo wa Mtakatifu Fransisko, akamwambia kwamba anataka kuiacha dunia apate kumtumikia Mungu kwa faragha. Mtakatifu Fransisko alimjaribu kwanza, akamtuma kwenda kuomba chakula chake kwa watu kama mtu maskini.  Klara alikataa kuchumbiwa mara mbili.

 

Wazazi wake walipotaka aposwe na kijana tajiri, wakati huo Klara akiwa na umri wa miaka kumi na nane, alitoka kisirisi nyumbani kwa baba yake. Siku ya sikukuu katika upweke, alienda katika Kanisa ya Porsiunkula akayavua mavazi yake ya umalidadi, na Mtakatifu Fransisko akazikata nywele zake na kumvika shela ya masista.

 

Wazazi wake walitaka kumrudisha nyumbani kwa nguvu, lakini Klara akawaambia ya kuwa hamtaki mchumba mwingine isipokuwa Yesu Kristu. Punde kidogo dada yake Anyesi alikuja kumtazama ili amgeuze Klara ili aibadili nia yake.

Lakini Klara akamshawishi dada yake na mwishowe, Anyesi mwenyewe akaingia utawa. Baada ya miaka michache hata mama yake alipokuwa mjane akaingia pia utawani. Huu ndio uliokuwa a mwanzo wa shirika la 'Waklara Fukara'. Watawa hawa waliishi maisha a magumu sana.

 

Kwa mujibu wa kanuni yao, walitembea kwa miguu mitupu, walilala chini, hawakula nyama maisha yao yote hata kule kuzungumza hawakuweza kuzungumza na mtu hadi hapo ilipobidi kufanya hivyo au ikiwa kwanza wanasemeshwa. Ilikuwa marufuku kwa Masista au Shirika lenyewe kumiliki mali ya aina yoyote. Lakini Klara alikuwa na busara ya kuwatunza Masista wake kwa hivi alimwandikia Mama Mkuu wa Konventi nyingine asiongeze mambo magumu zaidi "sababu miili yetu siyo ya chuma''.

 

Klara alipenda kusali karibu na Tabernakulo alimo Bwana wetu Yesu katika Sakramenti ya Ekaristi.

Mwenyewe alizishona nguo za kulipamba Kanisa. Siku moja Waislamu walishambulia mji wa Asisi, wakauteka walitaka kuingia kwa nguvu katika Monasteri ya Mtakatifu Klara. Ingawa Klara alikuwa mgonjwa, alitoka kitandani akaenda Kanisani, akatwaa chombo chenye Hostia Takatifu akapiga magoti katika mlango wa Monasteri, akasali hivi: "Mungu, usitoe roho zetu sisi tunaokutumainia kwa watu hawa wakali. Ulinde watumishi wako ulio wakomboa kwa damu yako". Ndipo Waislamu walishikwa na hofu wakakimbia kwa fujo.

 

Alikuwa Mkuu wa Shirika lake kwa muda ya miaka arobaini, akafariki dunia mwaka 1253, miaka ishirini na saba baada ya kufa kwa Fransisko wa Asizi. Alitajwa kuwa Mtakatifu mwaka 1255, miaka mitatu tu kisha kufa kwake.

 

Mtakatifu Klara Wa Asizi, mtawa na mwanzilishi wa shirika utuombee.

Post a Comment

Previous Post Next Post