MAISHA YA MTAKATIFU PAMAKIO (410)

Mtakatifu Pamakio Alizaliwa mjini Roma (Italia) zamani za mwaka 340 na alipofikia umri wa makamo akawa mbunge wa Dola ya Roma ndiyo hadhi ambayo zamani zile ilikuwa ya maana kubwa sana. 

zaidi ya kazi yake ya Ubunge alitumia muda mwingi kujifunza mambo mengi, akawa mwenye elimu kubwa.

Pia alijitolea kwa mambo ya dini na alikuwa na uhusiano wa kirafiki na Mtakatifu Jeronimo. 

Mke wake aliitwa Paulina ambaye mama yake alikuwa Mtakatifu Paula, mmojapo wa mabibi tajiri na wenye kumcha Mungu mjini Roma.

Mwaka 397 Pamakio alipofiwa na mke wake (huyo alikufa wakati wa kuzaa mtoto) aliandikiwa na Paulino, Askofu wa Nola barua ndefu ya kumpa pole.

Katika barua hiyo Askofu huyo aliandika kwamba mke wake marehemu sasa ni mwombezi wake mbele ya Bwana Yesu. 

Alisifiwa sana kwa ajili ya fadhila zake za imani, wema na uhodari. Mtakatifu Jeronimo alimwandikia Pamakio barua ya namna hiyo hiyo.

Tangu hapo Pamakio alijitolea kutenda mema mengi akitumia muda wake wote pamoja na mali yake. 

Katika utendaji huo alishirikiana sana na Mtakatifu Fabiola aliyekuwa mwanamke Mroma wa ukoo bora, naye tangu zamani aliwatembelea mara nyingi Pamakio na mke wake. 

Basi, hao wawili wakishirikiana waliweza kujenga hospitali na pia hosteli kwa ajili ya Mahujaji waliofika Roma kuhiji.

Mara nyingi hao wawili wenyewe waliwahudumia wakaaji wa nyumba hizo. 

Akiwasaidia wagonjwa, wenye kuteseka na mahujaji, Pamakio alizifuata nyayo za Paulina, mke wake marehemu. 

Kila alipoonekana mitaani mjini Roma, vipofu, maskini na walemavu walikuwa na hakika kwamba hatakataa kuwafariji kwa namna yoyote.

Alifariki dunia mwaka 410. Pamakio hakuwa Padre wala Mtawa, hata hivyo alishi Kikristo kabisa akiangalia Injili kama mwongozo katika maisha yake ya kila siku. 

Namna yake ya kuishi yatuonesha kwamba mtu aliye tajiri, msomi na mwenye hadhi, anaweza kabisa kuishi Kikristo kwelikweli, kujiwekea hazina mbinguni kwa kutenda mema mengi.


MTAKATIFU PAMAKIO, UTUOMBEE..

Post a Comment

Previous Post Next Post