Mtakatifu Yosefu Kalasanzi (1648)
 
Yosefu Kalasanzi alizaliwa Hispania mwaka 1557 na wazazi wa asili bora waliotoka katika ukoo wa wafalme wa Aragoni. Alipokuwa na umri wa miaka mitano alipenda kuigiza kazi ya maskari alitwaa upanga mdogo mikononi akisema kwa wenzake: "Haya, twendeni kupigana na mashetani". 
 Halafu alikusanya watoto karibu na altare aliyoijenga mwenyewe, akapanda juu ya kiti akaanza kuwafundisha katekismu. 

Alipokuwa kijana alitaka kufuata mfano wa Watakatifu, alijikatifu sana alilala juu ya mbao, alifunga mara kwa mara, alivaa shati gumu lenye nywele za kuwasha, alijipiga mijeledi ili azuie tamaa mbaya za mwili. Alipata elimu nzuri katika chuo kikuu alimosoma sheria na teolojia. Baadaye, alipadrishwa akawa mtume hodari aliwaongoza wakosefu wengi akakomesha ubishi na uadui na kuwapatanisha watu waliotaka kulipiana kisasi. 

Mfalme wa Hispania alitaka kumweka awe Askofu lakini Yosefu alisikia moyoni mwake sauti ya Mungu iliyomwambia aende Roma (Italia). Alipofika Roma, alizidi kusali na kufanya mema mengi. Usiku alishinda Kanisani mbele ya Sakramenti Kuu, mchana alikwenda kuwaangalia wagonjwa na kuwafariji wafungwa gerezani. 

 Kila siku ya Jumapili aliwakusanya watoto na kuwafundisha katekisimu aliwafundisha dini watumishi na mafundi na watu wa vijijini aliwahimiza kuungama na kupokea Ekaristi.

Wakati ugonjwa wa tauni ulipotokea huko Roma mwaka 1595 alijitolea akiwa na rafiki yake Mtakatifu Kamili wa Lelis waliwasaidia wagonjwa na wote waliokuwa katika hatua ya kufa.

Kwa muda wa miaka mingi padre Yosefu Kalasanzi alijitolea kuwafundisha watoto fukara. Alijenga shule kadhaa kwa ajili ya elimu iliyohitajika kwa watoto maskini humo waliweza kupata elimu bila malipo. 

Alianzisha Shirika la Kitawa kwa ajili ya shughuli hiyo ya kuwalea watoto hasa watoto yatima na maskini. Zaidi ya hayo kutokana na wivu wa wengine ilimpasa kuvumilia mateso mengi. Alifia Roma mwaka 1648 na alitangazwa Mtakatifu mwaka 1767. 

MTAKATIFU YOSEFU KALASANZI PADRE NA MWANZILISHI WA SHIRIKA, UTUOMBEE..

Post a Comment

Previous Post Next Post