DHAMIRI
"Dhamiri ni kiini cha binadamu cha ndani na siri kabisa, patakatifu ambamo mtu yu peke yake na Mungu na ambamo sauti yake yasikika."
Ndani kabisa ya dhamiri ya mtu, ipo sheria ambayo hakujiwekea mwenyewe, bali ambayo ni lazima aitii. Na sauti hiyo yasikika moyoni mwa mtu huyo wakati unaotakiwa na inayomwita kupenda na kutenda kilicho chema na kuepuka kibaya. kwani mwanadamu anayo sheria moyoni mwake iliyoandikwa na Mungu. (KKKT uk 414)
Dhamiri ni zaidi ya hisia, kwani hisia zetu si kamilifu na zinaweza kutuongoza vibaya. Kuna wakati hisia zetu zinaweza kuwa na nguvu sana kiasi cha kuathiri dhamiri yetu. (Yer 17:9) "Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?" Mfano mwingine mzuri; kabla ya Mtume Paulo kuongoka, aliwatesa vikali watu wa Mungu naye aliamini kwamba anafanya jambo zuri, kwani alihisi anatenda haki, lakini baadae aligundua kosa lake naye akakiri "Maana sijui sababu ya kujishtaki nafsi yangu, lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo; ila anihukumiye ni Bwana". (1Kor 4:4)
Kwa maelezo mengine, tunaweza sema kuwa, dhamiri ni mfano wa mtu wa ndani ambaye yeye anatusahihisha na kutushuhudia pale tunapotaka kufanya uovu.
DHAMIRI NA HUKUMU
Dhamiri ni hukumu ya akili ambamo mwanadamu hutambua sifa adilifu ya tendo halisi analoelekea kulitenda, angali akilifanya au amekwisha kulitekeleza, na ni katika yote asemayo na atendayo, mwanadamu hana budi kufuata kiaminifu anachojua kuwa ni haki na sahihi.
Hivyo, ni wito kwa kila mkristo kuwa karibu kiasi cha kutosha na nafsi yake mwenyewe ili aweze kuisikia na kuifuata sauti ya dhamiri yake, hitaji ambalo ni la lazima sana kwani maisha yetu mara nyingi yanavuruga tafakari yetu, na wakati mwingne kukosa muda wa kutafiti dhamiri zetu.
Je, nini hutokea pale tunapopuuza au kusikiliza dhamiri dhamiri zetu?
Tukumbuke kuwa, kila mmoja wetu anaweza kuchagua ikiwa ataisikiliza dhamiri yake au la. Adamu na Hawa waliamua hawatasikiliza dhamiri zao, na kwa sababu hiyo wakatenda dhambi. Baadae walijihisi wakiwa na hatia, lakini ilikuwa kwa kuchelewa mno, kwani tayari walikuwa wamemwasi Mungu. (Mwanzo 3:7)
Kwa upande mwingine, ipo mifano ya wale waliosikiliza na kutii dhamiri zao, Ayubu ni mfano mzuri. Alisikiliza dhamiri yake na kufanya maamuzi mazuri, naye alisema "Haki yangu naishika sana, wala sitaiacha; Moyo wangu hautanisuta wakati nikiwapo hai." Ayubu 27:6
Je, tunawezaje sasa kuzilea dhamiri zetu?
Ni kweli kuwa, katika kipindi fulani dhamiri yetu inaweza kutuongoza vibaya, kwani inaweza kupotoshwa na mawazo au hisia zetu zenye dhambi na kutuongoza kwa njia isiyofaa. Hivyo dhamiri njema huhitaji kulelewa na kuzoezwa. Baadhi ya njia hizo ni kama ifuatavyo;
- Kupitia neno la Mungu.
Neno la Mungu ni nuru na juu ya njia yetu. Tunapaswa kulitumia kwa imani, katika sala, kulitia katika utendaji na zaidi kumwomba Roho Mtakatifu kupitia mapaji yake atuongoze katika maamuzi yetu ya kila siku. (Warumi 9:1)
- Kupitia Mashauri na mafundisho ya Kanisa
Vile vile kupitia mashauri mema ya watu wengine, na mafundisho ya Kanisa yenye mamlaka, tunaweza kuzilea na kuzikuza dhamiri zetu katika misingi iliyo bora.
DHAMIRI KATIKA MAAMUZI
Binadamu mara kadhaa tunakabiliwa na hali zinazofanya hukumu za kimaadili zisizo na uhakika wa kutosha na uamuzi mgumu; lakini daima tunapaswa kutafuta kwa dhati kile kilicho na haki na chema na kupambanua mapenzi ya Mungu katika sheria yake.
Katika agani jipya, tukirejea; Mfano ule ambao mafarisayo na waandishi walipomkamata yule mwanamke katika uzinzi (Yoh 8:9) "Nao waliposikia, wakashtakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakinzia tangu wazee hata wa mwisho wao; Bwana Yesu aliwaambia maneno ambayo dhamiri zao wote ziliwachoma wakaondoka wakamuacha yule Mwanamke wasimpige mawe.
Katika nyakati kama hizo, sheria kadhaa hutumika katika kila jambo; (KKKT uk 416)
- Hairuhusiwi kamwe kutenda jambo baya ili kupata jambo jema.
- Kanuni ya dhahabu. "Yoyote mtakayo kutendewa na wengine, nanyi watendeeni vivyo hivyo" Mt 7:14
- Mapendo hupita daima kwa njia ya heshima ya jirani na dhamiri yake: "Hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kutia jeraha dhamiri iliyo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo." 1Kor 8:12
- "Ni vyema kutotenda neno lolote ambalo kwa hilo ndugu yako hukwazwa." Rom 14:21
Hivyo basi, dhamiri inapokabiliwa na uchaguzi mwema, yaweza kufanya hukumu sahihi kufuatana na akili, na sheria ya kimungu au, kinyume chake yaweza kufanya hukumu potofu inayojitenga na hali hizo.
Ikiwa kuna jambo unafanya na dhamiri yako inakushuhudia kuwa si sawa basi acha mara moja na dhamiri yako itakuwa i hai, kwa maana ya kuwa haijafa, lakini kama unaona unafanya uovu na huoni dhamiri ikikushtaki, basi jua dhamiri yako imekwisha kufa.
Basi ni wito kwetu sote daima kuitii hukumu ya kweli ya dhamiri yetu na tunaalikwa daima kutumia njia zinazofaa kulea dhamiri zetu ili zituongoze vyema katika maamuzi adilifu.
"Nami ninajizoeza katika neno hili niwe na dhamiri isiyo na hatia mbele za Mungu na mbele ya watu siku zote" Mdo 24:16
Tumsifu Yesu Kristo...
Post a Comment