Maisha ya Mtakatifu Agatha wa Sicilia
Mtakatifu Agatha, anayejulikana pia kama Agatha wa Sicilia, ni miongoni mwa mashahidi bikira wanaoheshimiwa sana katika Kanisa Katoliki. Inasadikiwa alizaliwa karibu mwaka 231 katika Catania au Palermo, Sicilia, katika familia tajiri na ya heshima.
Tangu akiwa mdogo, Agatha aliyekuwa mrembo sana aliweka maisha yake kwa Mungu. Alijitolea kuwa bikira mtakatifu, akichagua kubaki katika useja na kujitoa kikamilifu kwa Yesu na Kanisa kwa maisha ya sala na huduma. Hata hivyo, haikumzuia wanaume wengi kumtamani na kumfuata kwa tamaa zao zisizohitajika.
Miongoni mwao alikuwapo Quintianus, mtawala wa ngazi ya juu wa dola. Alidhani angeweza kumlazimisha Agatha aache nadhiri zake na kumuoa. Alipokataliwa mara kwa mara, Quintianus, akijua kuwa Agatha ni Mkristo katika kipindi cha mateso chini ya Kaisari Decius, alimkamata na kumpeleka mahakamani kwake yeye mwenyewe kama Jaji.
Alitarajia kwamba Agatha angebadilika akitishiwa kwa mateso na kifo, lakini yeye alibaki thabiti katika imani yake akisema:
“Yesu Kristo, Bwana wa wote, unaona moyo wangu, unajua matamanio yangu. Nimiliki mimi kikamilifu. Mimi ni kondoo wako: nifanye niwe mwaminifu kushinda majaribu ya shetani.”
Kwa machozi akimwomba Mungu ujasiri, aliendelea kushikamana na imani yake.
Mateso
Quintianus aliamuru afungwe gerezani katika nyumba ya makahaba ili kumdhalilisha na kumshawishi aache imani yake. Agatha, hata hivyo, hakupoteza matumaini, bali alibaki thabiti katika usafi na sala. Baada ya mwezi mzima wa kujaribiwa, bado alikuwa na nguvu ya kiroho, jambo lililomkasirisha zaidi Quintianus.
Aliporudishwa mbele ya Jaji, Agatha alisema kuwa mtumishi wa Kristo ndiko kulikuwa uhuru wake wa kweli. Kwa hasira, Quintianus akamrudisha gerezani na kisha akaamuru mateso makali: alivutwa kwa vyuma, kuchomwa kwa miale ya moto, na kuchapwa vibaya. Hatimaye, aliamuru matiti yake yakatwe.
Agatha alirudishwa gerezani bila chakula wala huduma yoyote ya kitabibu, lakini Bwana alimtunza. Katika maono, Mtume Petro alimtokea na kumfariji, akimponya majeraha yake kwa sala.
Baada ya siku nne, Quintianus aliamua kumpa mateso makali zaidi: Agatha alivuliwa nguo na kuwekwa juu ya makaa ya moto yaliyokuwa yamechanganywa na vipande vya chuma vyenye makali.
Akiwa gerezani tena, Agatha alisali:
“Bwana, Muumba wangu, tangu utotoni umenilinda; umenitoa kwenye upendo wa dunia, umenipa uvumilivu wa kustahimili mateso: sasa pokea roho yangu.”
Inasadikika kwamba Agatha alifariki na kuingia Mbinguni karibu mwaka 251.
Urithi na Heshima
Katika sanaa ya kidini, mara nyingi huonyeshwa akiwa na mkasi, vyuma vya mateso, au matiti yaliyowekwa juu ya sahani.
Mt. Agatha ni msimamizi (patron saint) wa:
-Sicilia na Palermo
-Wagonjwa wa saratani ya matiti
-Waathirika wa ubakaji
-Wakunga na wanyonyesha watoto
-Wanaopiga kengele
-Watu wanaokabiliwa na majanga ya moto
Sikukuu yake huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Februari.
Sala
“Mtakatifu Agatha, ulipitia udhalilishaji na mashambulizi ya kijinsia kwa sababu ya imani yako na usafi wako. Usaidie waponywe wote waliopitia unyanyasaji wa kijinsia na ulinde wanawake walio katika hatari. Amina.”
MTAKATIFU AGATHA, UTUOMBEE..
Post a Comment