MAISHA YA MTAKATIFU FRANSISKO WA ASIZI 
Mt. Fransisko wa Asizi alizaliwa mwaka 1181 au 1182 mjini Assisi-Italia. Fransisko alikuwa mtoto wa Petro Bernadone, mfanya biashara wa vitambaa vya nguo katika mji wa Asizi, Mama yake aliitwa Pika, alikuwa mama wa nyumbani na mcha Mungu. 

Petro alidhamiria kuwa mwanae wa kwanza angerithi kazi yake. Lakini Fransisko kwa namna yoyote hakuwa na uroho kama baba yake. Bali, alikuwa mkarimu sana na katika hali ya uchangamfu na cheshi alitoa chochote kilichokuwa chini ya mamlaka yake. 

Bwana wetu Yesu kristo, ambaye furaha yake ni kuonesha huruma kwa wenye huruma, alidhamiria kumwepusha Fransisko kutoka kwenye hatari ya starehe za kidunia na kumvuta kwake. Aliruhusu Fransisko augue sana. Akiwa amelala katika upweke wa chumba cha wagonjwa, akidhoofika kimwili, roho yake ilikuwa inaandaliwa na Mungu kwa mambo ya juu zaidi. Alijisikia hamu kubwa ya ukamilifu, na kujishinda kishujaa kulihitajika kama msingi wa ndoto hiyo. 

Siku moja baada ya kupona akiwa amepanda farasi akikatiza uwanda wa Asizi, alikutana na mkoma. Hali hiyo isiyotegemewa, ilimwogopesha, na alitaka kurudi nyuma. Lakini alikumbuka azimio lake, akateremka na haraka akabusu mkono wa yule mkoma na kuweka sadaka kwenye mkono wake. Alipopanda farasi tena na kugeuka ili amuage mkoma yule, hapakuwepo na mtu yeyote kwenye uwanda ule. Inaonekana Kristo alijionesha kwake katika umbo la mkoma. 

Fransisko aliwapenda mafukara kiasi kwamba mara nyingi alishirikiana nao. Pia akitimiza amri ya Mungu, aliomba mawe ya kukarabati Makanisa matatu yaliyokuwa yameharibika. Baba yake alikasirishwa sana na mwenendo huo wa ajabu na kuamua kumpeleka mwanae mbele ya Askofu wa Asizi. Hapo Fransisko hakumrudishia tu baba yake pesa alizokuwa nazo, bali hata nguo alizokuwa amevaa akisema: "Sasa hakika naweza kusema, Baba yetu uliye mbinguni". 

Askofu alimpa joho kuukuu la mtunza bustani, ambalo kwa nyuma Fransisko alichora Msalaba kwa kipande cheupe cha chaki. Kuanzia wakati huo alimwomba Bwana Yesu mapenzi yake kuhusu mambo yajayo katika maisha yake. Muda si mrefu, Fransisko akiwa kwenye Misa Takatifu huko Portiuncula, alisikia Injili ambapo Bwana wetu anawatuma mitume wake na kuwaambia wasichukue wala dhahabu, wala fedha, wala makoti mawili, wala viatu. Moyo wa Fransisko ulijazwa furaha, kwani aling'amua mapenzi ya Mungu kuhusu maisha yake. Akiwa amevaa vazi la toba, kwa mshipi, na bila viatu, alianza maisha ya ufukara halisi na kuanza kuhubiri toba. 

Hii ilitokea Mwaka 1208, akiwa na umri wa miaka 26 hivi.
Mara wenzi kadhaa wakajiunga naye. Walipofikia kumi na moja, aliongozana nao kwenda Roma, ambapo Papa Innosenti wa III alitoa idhini yake kwa Shirika jipya. Waliishi katika ufukara halisi na katika uelewano wa kidugu, wakihubiri toba kwa watu kwa matendo na maneno yao.
Mwanzilishi Mtakatifu Fransisko aliwaita Ndugu Wadogo, ili daima wathamini karama ya unyenyekevu kama msingi wa ukamilifu. Yeye mwenyewe alikuwa mnyenyekevu kiasi kwamba watu walipomwita Mtakatifu, alijiita mdhambi mkubwa, "Kwani," alisema, "kama Mungu angempa mhalifu mkubwa zaidi neema alizonijalia mimi, angeweza kuzitumia kwa faida kubwa zaidi kuliko mimi nilivyofanya". 

Hata hivyo hamu yake ya kuunganika zaidi na Mungu ilimsukuma tena na tena ajitenge na kukaa upwekeni kwa ajili ya kufunga na kusali. Aliwaka moto wa upendo kwa Mungu Mkuu na aliye juu. "Katika uzuri wa vitu," anasema Mtakatifu Bonaventura, "aliona Muumbaji wa uzuri wote, na alifuata nyayo za mpendwa wake aliyetia chapa ya taswira yake katika viumbe vyote". Akiwa amejaa upendo aliweza kualika viumbe vyote vimsifu Muumba pamoja naye, na ndege waliungana naye kuimba nyimbo za kumsifu Mungu. 

Zaidi Fransisko alimtambua Mwokozi, Yesu Kristo katika uso wa kila mmoja aliyekutana naye na kwa namna ya pekee mafukara, na wote walioteseka kutokana na mfumo wa kukosewa haki, kunyanyaswa, kusulubiwa kwa hali yoyote ile, (yaani aliweza kumhudumia kristo ndani ya maisha yao, tena kwa furaha kuwa isiyo na maelezo.) Aliwapokea hao wote na kuwapa heshima stahiki. Fransisko alikuwa ni mtu mwenye maono, hata pale alipokuwa kwenye mahandaki (kipindi alipokuwa mfungwa wakati wa vita mjini Assisi) akiamini kwamba mwisho wa handaki kuna mwanga aliamini kwamba kuna alfajiri baada ya usiku. 

Kama mkristo kweli, alithibitisha kwamba lengo pekee la kuishi hapa duniani si kingine ila ni kudhihirisha upendo wetu kwa Mungu na jirani zetu hususani wale wahitaji. Furaha kubwa ilikuwa ni kumtumikia kristo katika walio wadogo na walioachwa na jamii. 
Zaidi ya yote ilikuwa ni mateso na kifo cha Kristo Msalabani ambavyo viliujaza moyo wake upendo wa Mkombozi wake, na alijitahidi kadiri alivyoweza kufanana na Kristo msulubiwa. Miaka miwili kabla ya kifo chake, katika mlima La Verna, Mwokozi msulubiwa alimtokea Fransisko katika umbo la kiserafi na kumpatia chapa ya Madonda Matano Matakatifu kwenye mwili wake.

Fransisko alijua mapema siku ya kifo chake. Ingawaje kilitanguliwa na maumivu makali, alimshukuru Mungu kwa ajili hiyo na kusema wazi wazi kuwa yupo tayari kuteseka hata mara mia zaidi kama ni mapenzi ya Mungu.

Akiwa amefarijiwa kwa Sakramenti zote za Kanisa Takatifu, na akiwa amelala juu ya ardhi kwa mfano wa kifo cha Mkombozi Msalabani, Fransisko alikwenda makao yake ya mbinguni tarehe 3 Oktoba 1226. Alitangazwa Mtakatifu tarehe 16, Julai, 1228 na rafiki yake Papa Gregori IX. 

Mt. Fransisko wa Asizi, kupitia maisha yake hapa duniani alituachia karama saba (07) ambazo kama wakristo ni wito kwetu kuzitumia katika kuuishi ukristo wetu hapa duniani, nazo ni; Ukarimu (upendo), uyenyekevu, udogo, utii, ufukara, sala na zaidi kuishi Maisha ya Jumuiya. 

MTAKATIFU FRANSISKO WA ASIZI, UTUOMBEE..

Post a Comment

Previous Post Next Post