MAISHA YA MTAKATIFU YOSEFU WA KOPERTINO, PADRE (1663)
Yosefu alizaliwa mwaka 1603 na wazazi maskini.
Alizaliwa katika zizi la ng’ombe, katika mazingira yaliyofanana sana na yale ya Mwokozi alipozaliwa.
Hakuwa na nafasi ya kwenda shule ili kujifunza kusoma na kuandika.
Alipokuwa bado mtoto, mara kwa mara wazazi wake walimkuta kanisani amepiga magoti kwenye daraja la altare. Alitulia tuli pasipo kujitikisa hata kidogo, macho yake yakiwa yameelekezwa kwenye tabernakulo akimtazama Yesu Kristo kwa fikara ya rohoni. Mara nyingi alikamatwa katika hali hiyo kwa muda wa saa nzima bila kugeuka hata mara moja.
Alipotimiza umri wa miaka kumi na saba, akaamua kuacha dunia na akaenda kupiga hodi mlangoni pa monasteri ya Wamonaki wa Mtakatifu Fransisko. Humo alipewa kazi za kufagia banda la punda na kazi nyingine za kawaida. Alizikubali kwa moyo wote na akasifiwa kwamba alikuwa mcha Mungu.
Walipomwona akifunga kila siku, akilala usiku juu ya ngozi ya mnyama iliyotandikwa kwenye mbao tatu, na kila tendo lake likiambatana na sala, wakagundua kuwa alikuwa tayari kutumwa popote na kufanya kazi ngumu kwa upendo. Wale waliokuwa wakimdharau hapo awali walianza kumpa heshima.
Siku ya mitihani ya wanafunzi waliokuwa wamemaliza mafunzo yao, walimu wakuu walishauriana kumwita Yosefu ili wapime akili yake, labda akafaa kusomeshwa. Wote walikubaliana kwamba alikuwa mtu wa utakatifu na aliyefaa kuwa Padre.
Walipomwuliza maswali, walishangaa mno kumwona akiyajibu kwa uelewa mkubwa. Walipomuuliza vipi alifanikisha hayo ilhali hakujua kusoma, akasema: “Aliyenisaidia ni Bikira Maria niliyemwomba ili nipate kuwa Padre.”
Hapo wakuu wakaamuru apewe daraja ya Upadre pamoja na wenzake.
Baada ya kuwa Padre, Yosefu aliendelea kukua katika hali ya utakatifu, roho yake ikimwaza Mungu kila dakika. Mara nyingi alionekana amesimama kimya kama sanamu, asihisi kuguswa wala kuitwa.
Japokuwa Yosefu aliwaponya wagonjwa wengi kwa miujiza, anatambulika zaidi kwa tukio la kuelea angani wakati wa sala. Alionekana mara nyingi zaidi ya sabini akiwa katika hali hiyo mbele ya watu wengi, na habari hizi zikaandikwa rasmi.
Mara moja, akiwa bado hai, kanisani mbele ya waumini, Yosefu alipaa juu ya vichwa vyao akielekea sanamu ya Bikira Maria. Alisali kwa muda akiwa angani, kisha akarudi chumbani kwake huku akiendelea kuelea.
Hatimaye aliposhikwa na homa alijua kwamba saa yake ilikuwa imewadia. Alifariki akiwa anabusu msalaba wake mdogo na akiyatamka majina ya Yesu na Maria.
Alifariki mwaka 1663 na alitangazwa kuwa Mtakatifu mwaka 1767.
MTAKATIFU YOSEFU WA KOPERTINO, UTUOMBEE.
Post a Comment