![]() |
Mtume huyu wa Mapendo ya kindugu alizaliwa mwaka 1581 katika nchi ya Ufaransa. Wazazi wake walikuwa wakulima,na alipokuwa bado Mtoto, Baba yake alizoea kumtuma Vinsenti kuchunga mifugo yao malishani. Toka Utoto wake alikuwa na tabia njema ya kuwahurumia maskini, alipowahi kuwakuta njiani, aliwagawia unga aliokuwa nao mfukoni mwake. Baba yake alipouona mwenendo huu bora, akamwachisha kazi ya kuchunga na akampeleka kujifunza utawani ili apate kuwa Padre. Alisema ;’’Vinsenti atakuwa Padre mwema kwani ana moyo wa huruma’’.
Alipopata Upadre,Vinsenti akateuliwa kuwa Paroko wa Kanisa mojawapo mjini Paris (Ufaransa). Miaka michache baada ya kupadirishwa,mwenyewe alisema kwamba Padre Vinsenti alikuwa hana lengo ila tu kuwa padre mwema,na kuishi maisha bila shida. Lakini baada ya kuishi mjini Paris kwa muda wa miaka Kumi hivi,alipoona kwamba watu wa shambani walikuwa hawajui vema mafundisho ya dini, alianza kuwashugulikia zaidi.
Alienda kuwafundisha Katekisimu pamoja na Mapadre waliiopenda kazi hii, na hivyo pole pole waliliunda Shirika lao,ndilo Shirika la ‘Mapadre wa Misioni’,wanaoitwa pia Wavinsenti au Walazaristi. Shirika hilo lilikuwa na jukumu la kuleta mapinduzi katika maisha ya Kiroho ya Mapadre na pia kuwasaidia maskini.
Zaidi ya hayo,alikusanya jamii ya wanawake wengi wenye kazi ya kutunza maskini na kuuguza wagonjwa hospitalini. Alisaidiwa na Mt.Lusia wa Mariyak katika kuanzisha shirika la ‘mabibi wa Upendo’. Licha ya hayo,padre Vinsenti alikusanya watoto wa haramu walioachwa njiani na mama zao,akashugulika kuwalea kikristu. Alifaulu kuzitekeleza kuyatimiza kazi hizo zote kwa sababu alikuwa mtu wa imani,mtu wa mapendo kwa Yesu Kristu na kwa watu. Alichukia majivuno,na katika matata yote aliutumaini msaada wa Mungu.
Alikufa huko Paris mwaka 1660,akatajwa Mtakatifu mwaka 1737,naye Papa akamchagua awe msimamizi wa mashirika ya misaada. Mojawapo ya mashirika hayo ni shirika la Mtakatifu Vinsenti wa Paulo,lililoanzishwa na Frederiko Ozanam,huko Paris mwaka 1833.
Haya ndio maisha ya Mtakatifu Vinsenti wa Paulo Padre na Mwanzilishi wa Shirika kwa mujibu wa kitabu cha Watakatifu
MTAKATIFU VINSENTI WA PAULO, UTUOMBEE..
Post a Comment