MASOMO YA MISA, AGOSTI 27, 2024

JUMANNE, JUMA LA 21 LA MWAKA

KUMBUKUMBU YA MT. MONIKA

SOMO 1
2The. 2:1 – 3, 14 – 17

Tunakusihini ndugu, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo. Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yoyote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uaharibifu.

Bwana aliwaita ninyi kwa injili yetu, ili kuupata utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, ndugu, simameni imara, mkayashike mapokeo mliyofundishwa, ama kwa maneno, ama kwa waraka wetu. Na Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa faraja ya milele na tumaini jema, katika neema, awafariji mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 96:10 – 13 (K) 13

(K) Bwana anakuja aihukumu nchi.

Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki,
Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike,
Atawahukumu watu kwa adili. (K)

Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo.
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
Mbele za Bwana, kwa maana anakuja.
Kwa maana anakuja aihukumu nchi. (K)

Atahukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake. (K)


SHANGILIO
Lk. 8:15

Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno la Mungu, na kulishika. 
Aleluya.


INJILI
Mt. 25:23 – 26

Yesu alisema, Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka na mnanaa na bizari na jira, lakini meacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia.
Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang’anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.

Post a Comment

Previous Post Next Post