Masomo ya Misa 01/03/2025
Somo la Kwanza
YbS 17:1–15
Bwana alimwumba Adamu katika mavumbi, an hata mavumbini akamrudisha. Akawapa wanadamu siku kwa idadi, na muhula iliyoamriwa; akawapa amri juu ya vitu vilivyomo; akawavika nguvu kama Yeye mwenyewe, na kuwafanya kwa mfano wake. Akaitia hofu ya binadamu katika vyote vyenye mwili, ili wawatawale wanyama na ndege. Akawajaza maarifa ya hekima, na kuwapa kupambanua wema na uovu. Akawafanyizia ulimi, na macho, na masikio, akawapa na moyo wa ufahamu. Ili kuwaonyesha adhama ya kazi yake, ili wajisifie katika miujiza yake, na kukijulisha kicho chake ulimwenguni, na kulihimidi jina lake takatifu; aliyaweka mbele yao maarifa, akawapa sheria ya uzima kuwa urithi. Alifanyana na wateule wake agano la milele, na kuwaonyesha hukumu zake. Kwa macho yao waliiona enzi ya utukufu wake, na kwa masikio yao waliisikia sauti yake yenye nguvu. Akawaambia, Jihadharini na yasiyo haki, akawapa amri kila mtu juu ya jirani yake. Njia zao nazo zi mbele zake daima, wala hazitafichwa machoni pake.
Neno la Bwana, Tumshukuru Mungu
Wimbo wa Katikati
Zab 103:13-18
Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake,
Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao.
Kwa maana Yeye anatujua umbo letu,
Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.
(K) Fadhili za Bwana zina wamchao tangu milele hata milele.
Mwanadamu siku zake zi kama majani;
Kama ua la kondeni ndivyo asitawivyo.
Maana upepo hupita juu yake, kumbe haliko!
Na mahali pake hapatalijua tena.
(K) Fadhili za Bwana zina wamchao tangu milele hata milele.
Bali fadhili za Bwana zina wamchao Tangu milele hata milele,
Na haki yake ina wana wa wana;
Maana, wale walishikao agano lake,
Na kuyakumbuka maagizo yake ili wayafanye.
(K) Fadhili za Bwana zina wamchao tangu milele hata milele.
Shangilio
Zab 130:5
Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja Bwana, na neno lake nimelitumainia.
Aleluya.
Somo la Injili
Mk 10:13–16
Makutano walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukuzwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.
Neno la Bwana, Sifa kwako Ee Kristu
Post a Comment