UFAHAMU UGONJWA SUGU WA FIGO (Chronic Kidney Disease–CKD)
Makala hii imeelezwa katika vipengele vifuatavyo:
- Maana ya ugonjwa sugu wa figo
- Namna ugonjwa sugu wa figo hutokea
- Dalili za ugonjwa sugu wa figo
- Vihatarishi vya ugonjwa sugu wa figo
- Athari za ugonjwa sugu wa figo
- Matibabu na namna ya kukabiliana na ugonjwa sugu wa figo.
Maana
ya ugonjwa sugu wa figo.
Ugonjwa
sugu wa figo ni upungufu wa ufanyaji kazi wa figo unaodumu kwa zaidi ya miezi
mitatu . Figo za binadamu zinaposhindwa kufanya kazi zake vizuri kwa zaidi ya
asilimia sitini (60%) katika kipindi
kisichopungua miezi mitatu basi huweza kusababisha ugonjwa sugu
wa figo hata kupelekea figo hizo
kushindwa kabisa kufanya kazi kama
tatizo hilo halitatibiwa mapema. Miongoni mwa kazi muhimu za figo ni pamoja na
kuchuja damu ili kutoa takamwili za ziada kwa njia ya mkojo, husaidia
utengenezaji wa selidamu, kutengeneza vitamini D katika mwili ambayo husaidia
unyonyaji wa madini ya kalsiamu kutoka mfumo wa chakula pamoja na uratibu wa
kiwango cha maji na madini chuma mwilini.
Je,
ni kwa namna gani ugonjwa huu hutokea?
Binadamu ana figo mbili upande wa kulia na kushoto chini ya mbavu upande wa mgongoni. Kila figo moja ina vichujio vidogo vidogo (nephrons) zaidi ya milioni moja ambavyo ndiyo hufanya kazi ya kuchuja damu . Uharibifu wa vichujio hivyo husababisha figo kushindwa kuchuja damu vizuri, tatizo hili likidumu kwa muda mrefu huleta tatizo sugu la figo kushindwa kufanya kazi ipasavyo kwani vichujio hivyo vikiharibiwa haviwezi kurekebishwa au kuzalishwa tena. Katika maana hiyo ugonjwa huu huanza taratibu kulingana na kiwango cha uharibifu wa vichujio na kuwa hatari zaidi kadiri uharibifu unaopoendelea kuongezeka hadi kufikia kiwango cha figo kushindwa kufanya kazi zake tena na hapo ndipo tunapata tatizo la figo kufeli (kidney failure).
Uwezo wa figo kufanya kazi hupimwa kwa kiwango cha protini kwenye damu na mkojo (albumin na creatinine), Kiwango cha mkojo unaopatikana kwa muda maalumu pamoja uwezo wa figo kuchuja damu kupitia vichujio vyake.
Mgonjwa mwenye tatizo la figo hupoteza kiasi
kikubwa cha protini kwa njia ya mkojo, huwa na
damu kwenye mkojo pamoja na upungufu wa upatikanaji wa mkojo. Dalili hizi
zikidumu kwa zaidi ya kipindi cha miezi mitatu ndio tunapata dhana ya ugonjwa
sugu wa figo au kitaalamu unaitwa Chronic Kidney Disease (CKD).
Dalili
za ugonjwa sugu wa figo ni zipi?
Ugonjwa sugu wa figo una hatua tano na dalili zake huongezeka kadiri ugonjwa huo unapoendelea katika hatua kubwa zaidi. Mgonjwa anapofikia hatua ya tano ya ugonjwa basi figo zake haziwezi kufanya kazi yake na huhitaji matibabu mbadala kama uchujaji wa damu kwa mashine (Dialysis) au kupandikizwa figo kutoka kwa mtu mwingine.
Miongoni mwa dalili za ugonjwa sugu wa figo ni kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku, kupata maumivu wakati wa kukojoa na baadae unaweza kukosa mkojo kabisa, kichefuchefu, kupata mkojo wenye damu, kuwashwa mara kwa mara, kutapika, kukakamaa kwa misuli, miguu, tumbo au mwili mzima kuvimba, kupumua kwa shida, kupata maumivu ya tumbo, kutetemeka miguu na mikono na kupata kuchanganyikiwa. Ni muhimu tuonapo dalili kama hizo kuchukua hatua ya kumuona daktari kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Vitu gani vinatuweka katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa sugu wa figo?
Watu wenye shinikizo la juu la damu (hypertension), kisukari, uzito mkubwa (obesity), uvutaji wa sigara, kiwango kingi cha mafuta mwilini, unywaji wa pombe kali, magonjwa yanayosababishwa na kinga mwili, watu wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI, saratani hasa ya shingo ya kizazi, homa ya ini, umri mkubwa, historia ya magonjwa ya figo katika familia, magonjwa ya kurithi kama selimundu na magonjwa ya figo, matumizi holela ya dawa, maambukizi ya mara kwa mara katika figo pamoja na uzibaji wa njia ya mkojo wana uwezekano mkubwa wa kupata tatizo hili.
Aidha; mtu yeyote anaweza pata ugonjwa huu hivyo ni muhimu kuchunguza afya ya figo zetu mara kwa mara hasa tuonapo dalili za tatizo la figo.
Athari za ugonjwa sugu wa figo ni zipi?
Ugonjwa
sugu wa figo husababisha mwili kushindwa kutoa takamwili (urea) na maji ya
ziada pia baadhi ya homoni na kemikali
za mwili zinazozalishwa na figo hukosekana hivyo hupelekea mwili kushindwa kufanya
kazi ipasavyo. Miongoni mwa madhara ya ugonjwa huu ni pamoja na kupata
shinikizo la juu la damu, mwili kuvimba, kuvimba kwa ini na bandama hata ini
kushindwa kufanya kazi, mapafu kujaa maji na
kupumua kwa shida, kukosa madini ya kalsiamu, kuwa na kiwango kikubwa cha
madini ya fosforasi, kuziba kwa mishipa ya damu na misuli kukakamaa, kushuka kwa
kiwango cha damu, maumivu ya mifupa na kufeli kwa kazi ya uroto wa damu, kupata matatizo ya
moyo hasa moyo kushindwa kufanya
kazi (Heart failure), kutapika, kichefuchefu, kukosa mkojo, mwili kupata
ganzi, kupata maambukizi ya mara kwa mara kwasababu ya kinga ya mwili
kudhoofika, hitilafu za mfumo wa uzazi, figo kufeli na hata kupoteza maisha. Aidha ugonjwa huu
husababisha kuongezeka kwa gharama za matibabu kwa mgonjwa hasa kwa wale wenye
kipato cha chini na kusababisha
kuzorota kwa uchumi wa mtu binafsi pamoja na upotevu wa nguvu kazi ya jamii na
taifa kwa ujumla.
Matibabu na namna ya kukabiliana na ugonjwa sugu wa figo.
Matibabu
ya ugonjwa sugu wa figo hutegemea na hatua ya ugonjwa kwani ni rahisi zaidi
kutibu ugonjwa huu ukiwa katika hatua za awali. Ugonjwa huu unapofikia hatua ya
nne na ya tano huwa ni ngumu kutibika. Kwa kawaida matibabu yake huzingatia
kutatua chanzo kikuu kinachopelekea ugonjwa huu ikiwa ni pamoja matibabu ya
shinikizo la juu la damu, kisukari, magonjwa ya kinga ya mwili na magonjwa
mengine yanayopelekea ugonjwa huu.
Aidha
mgonjwa huweza kutibiwa madhara yanayoletwa na ugonjwa huu kama kurekebisha
kiwango cha madini mwilini hasa kalsiamu na fosforasi, kurekebisha kiwango cha
damu, kupunguza maji mwilini (Paracentesis/thoracocentesis) pamoja na
kupunguza kiwango cha maji na madini chumvi yanayoingia mwilini. Ugonjwa huu
unapofikia hatua ya tano ambapo figo zote hufeli, matibabu ya kusafisha damu mara kwa mara (Dialysis) au
kupandikizwa figo hufanyika. Ifahamike kuwa sheria za nchi yetu zinaruhusu
mchangiaji wa figo
kwa ajili ya matibabu ni lazima awe ndugu wa mgonjwa na awe ameridhia mwenyewe
kufanya hivo.
Matibabu ya kusafisha damu (Dialysis)
Tunaweza
kuepuka ugonjwa huu hasa kwa kupunguza chumvi na mafuta katika chakula, kufanya
uchunguzi wa mara kwa mara wa shinikizo
la damu na sukari mwilini, kupunguza unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara,
kuepuka matumizi holela ya dawa na kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara. Kwa
ujumla ni muhimu kujijengea tabia ya kuchunguza afya zetu mara kwa mara pamoja
na kuwaona wataalamu wa afya pale tuonapo dalili za ugonjwa huu ili kuweza
kuutibu katika hatua za awali. Jamii inapaswa kuelimishwa zaidi ili kujua namna
unavyoweza kupata tatizo la ugonjwa sugu wa figo na kuchukua tahadhari za mapema katika
kukabiliana na kujikinga
na ugonjwa huu.
Tumsifu Yesu Kristo...
Na Justin Godlove (Mwanafunzi wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili–MUHAS)
Post a Comment