Makala hii imegawanyika katika vipengele vifuatavyo;
- Utangulizi
- Ishara muhimu katika adhimisho la Misa Takatifu
- Mwanzo wa Misa Takatifu
- Liturjia ya neno
- Liturjia ya Ekaristi Takatifu
- Hitimisho la Misa Takatifu
Utangulizi
Misa Takatifu, ni tendo katika Roho Mtakatifu, la Kristo mwenyewe na kanisa lake katika kumtukuza na kumwabudu mwenyezi Mungu. (KKK)
Kwa kuwa adhimisho la Misa kwa hulka na hali yake ni tendo la "kijumuiya", viitikizano (dialogia) kati ya kuhani na waamini waliokusanyika, na pia mashangilio ya shangwe (acclamationes), vina maana sana. Hivo hizi si ishara za nje tu za adhimisho la kijumuiya, bali zinajenga na kukuza uhusiano wa muungano wa ndani (communio) kati ya kuhani nasi waamini, yaani liturjia.
- Mashangilio au/na vifijo, na viitikizano vya waamini kujibu maamkiano na sala za kuhani, ndivyo vinafanya ile hatua ya ushiriki kimatendo, hatua ambayo katika Misa ya aina yoyote, ni lazima itimilizwe na waamini waliokusanyika, ili kuonyesha na kukoleza utendaji wa jumuiya yote.
Sehemu nyingine zinazofaa sana kuonyesha na kukuza ushiriki wa waamini kimatendo, na ambazo zinahusisha jumuiya nzima iliyokusanyika, ni hasa tendo la kutubu (nakuungamia), kukiri imani (nasadiki); sala kwa ajili ya mahitaji yote (sala za waamini); na sala ya Bwana (Baba yetu).
Hivo basi, ipo tofauti kubwa kati ya kushiriki liturjia ya adhimisho la Misa Takatifu na kuhudhuria Misa, ambapo lililo sahihi ni kushiriki. Hivo basi kushiriki huku kunakuja pale tunapoleta uhai katika Adhimisho kwa kutimiza pale tunapohusika kwa matendo na ishara zote kiliturjia na kwa umaana wake.
Ishara Muhimu katika Adhimisho la Misa Takatifu.
- Kusimama: Kusimama kunaonyesha kiwango maalum cha heshima na utayari, kwa mfano, wakati wa usomaji wa Injili. Pia ni mkao wa kawaida wakati wa kuimba au wakati wa kuomba pamoja.
- Genuflection (kupiga goti moja): Genuflection hufanywa kwa kukunja goti la kulia chini. Inatolewa kwa Sakramenti Takatifu wakati wa kuingia au kutoka kanisani au wakati wa kupita mbele ya Tarbenakulo. Kwa kuongezea, kitendo hichi hufanywa wakati wa kukiri Umwilisho au kifo cha Kristo.
- Busu: Kidesturi, ishara hii ya Heshima hutolewa kwa kitabu cha Injili na Altare mwanzo na mwisho wa Adhimisho la Misa Takatifu.
- Kuinama sana: Ishara hii huelekezwa altareni wakati wowote mtu anapopita mbele yake wakati wa Misa na wakati wa kukiri Imani kwa maneno yanayorejelea moja kwa moja Umwilisho: "Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, alizaliwa na Bikira Maria, akawa mwanadamu.”
- Kuinamisha kichwa: Ishara hii hufanywa wakati wa Misa linapotajwa jina la Yesu, Nafsi tatu za Mungu jina la Maria, jina la mtakatifu ambaye kwa heshima yake Misa inaadhimishwa.
- Kuketi: Kuketi kunamaanisha usikivu, hasa kwa usomaji wa Maandiko Matakatifu au wakati wa matayarisho ya madhabahu.
- Kupiga magoti: Kupiga magoti yote mawili kunaashiria kumwabudu Mungu na unyenyekevu mbele zake. Ni mkao ufaao kwa kusanyiko wakati wa Sala ya Ekaristi, na baada ya wimbo wa Mwanakondoo kabla ya kupokea Komunyo Takatifu.
Mwanzo wa Misa
Waamini wakiisha kusanyika, wakati kuhani anapoingia pamoja na shemasi na watumishi, wimbo wa kuingia unaanzishwa. Lengo la wimbo huo ni kufungua adhimisho, kuimarisha umoja wa waliokusanyika, kuelekeza mioyo na akili zao kwenye fumbo la kipindi flani cha liturujia.
Mara baada ya Misa kuanza na kufuata kanuni za kiliturjia kiutangulizi, hufuata tendo la toba ambapo kuhani huwaalika watu wafanye tendo la toba, ambalo baada ya kitambo kidogo cha ukimya, hutimizwa kwa fomula ya maungamo ya jumla, na kuhitimishwa kwa maneno ya maondoleo yasemwayo na kuhani. Maneno haya lakini hayana nguvu ile ya Sakramenti ya Kitubio. (hivo si mbadala wa Sakramenti ya Kitubio, bali huwa ni ishara ya unyenyekevu kwa kukiri kuwa sisi tu wakosefu)
Baada ya Utukufu, (Utukufu ni utenzi wa kale sana na wenye kuheshimiwa sana, ambamo Kanisa linalokusanyika katika Roho Mtakatifu, humtukuza Baba na Mwana kondoo,) kuhani huwaalika watu kuomba. Na wote, pamoja na kuhani, wanakaa kimya kwa muda mfupi ili wajitambue kuwa wako mbele ya Mungu, na pia waweze kufanya maombi yao ya pekee moyoni. Ndipo kuhani anasema ile sala ambayo tumezoea kuiita Kolekta. Kwani kwa sala hii, hali au mwelekeo wa adhimisho unatambulishwa. Kutokana na mapokeo ya zamani ya Kanisa, kwa kawaida sala hiyo huelekezwa kwa Mungu Baba kwa njia ya Yesu Kristo katika Roho Mtakatifu, na hufungwa kwa hitimisho linalotamka Utatu Mtakatifu.
Liturjia ya Neno
Liturjia ya Neno huundwa hasa na mkusanyiko wa Masomo, zaburi pamoja na Injili.
- Liturjia ya Neno huambatana na vipindi flani vya ukimya na tafakari. Kwa njia ya vipindi hivyo na kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, Neno la Mungu linapokewa moyoni, na jibu lake linaandaliwa moyoni lipate kutolewa kwa njia ya sala. Vipindi vya ukimya vinaweza kufanyika na kuleta manufaa, kama kabla ya kuanza Liturujia yenyewe ya Neno, baada ya somo la kwanza na la pili, na baada ya homilia kutolewa.
Baada ya kila somo, msomaji hutamka mwaliko, ambao watu waliokusanyika wanajibu. Na hivyo wanatoa heshima kwa Neno la Mungu, walilolipokea kwa imani na moyo wa shukrani. Somo la Injili ndiyo kilele cha Liturujia ya Neno. Liturujia yenyewe inatufundisha kwamba ni lazima somo la Injili lipewe heshima ya kipekee kuliko masomo mengine. Heshima hiyo hujitokeza kwa upande wa mhudumu aliyepewa jukumu la kuitangaza kupaswa kuomba baraka, au kusali sala ili kujiandaa. Na heshima hiyo hujitokeza vilevile kwa upande wa waamini wanaotambua na kuungama kwa njia ya viitikio vya kupongeza (wimbo wa Aleluya) kwamba Kristo yupo hapohapo na kusema nao; nao wanasikiliza somo la Injili hali wamesimama. Mwishowe heshima hiyo inaonekana kwa ishara za heshima zinazotolewa kwa kitabu cha Injili. (Busu lakuhani kwa kitabu)
Mara baada ya Liturjia ya neno kumalizika, Hufuata tendo la kukiri Imani na maombi, ikiwa kama maandalizi kwa ajili ya Liturjia ya Ekaristi. Kanuni ya Imani, au “Symbolum” yaani Ungamo la Imani linaelekeza hivi: Taifa lote la Mungu lililokusanyika pamoja, waliitikie Neno la Mungu lililotangazwa katika masomo ya Maandiko Matakatifu na kufafanuliwa katika homilia. Tena, watu haohao wakiisha tamka Kanuni ya Imani kwa kutumia fomula iliyoidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya liturujia, huyakumbuka mafumbo makuu ya imani, na kuyaungama, kabla hawajaanza kuyaadhimisha katika Liturujia ya Ekaristi.
Katika maombi kwa wote au Sala ya Waamini, watu wa Mungu huliitikia Neno la Mungu walilolipokea kwa imani; na, kwa kutekeleza wajibu wa ukuhani wao utokanao na Ubatizo, (1Petro 2:9) wanamtolea Mungu maombi kwa ajili ya wokovu wa watu wote. (Kwa kawaida ni vema maombi ya namna hiyo yafanywe katika Misa pamoja na watu, kwa ajili ya Kanisa takatifu, kwa ajili ya wale wanaotutawala, kwa ajili ya wale wanaosumbuliwa na shida mbalimbali, na kwa ajili ya watu wote na wokovu wa ulimwengu mzima.)
Liturjia ya Ekaristi
Katika Karamu ya mwisho, Kristo aliweka sadaka na karamu ya kipasaka. Kutokana na hilo, sadaka ya msalaba inafana iwepo siku zote katika Kanisa, kila mara ambapo, kuhani akimwakilisha Kristo Bwana, hufanya kilekile na kwa namna ileile alivyofanya Bwana mwenyewe, na akawakabidhi wanafunzi wake wafanye vile kwa ukumbusho wake. Kwa maana, Kristo alitwaa mkate na kikombe, akashukuru, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, "Twaeni, mle, wote; huu ndio Mwili wangu; hiki ndicho kikombe cha Damu yangu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi”. (Tokea hapo, Kanisa limeshikilia na kuratibu adhimisho lote la Liturujia ya Ekaristi katika sehemu zake lilingane na maneno na matendo hayahaya ya Kristo mwenyewe.) Kutokana na hayo:
- Katika maandalizi ya vipaji, mkate na divai pamoja na maji huletwa altareni, yaani vitu vilevile Kristo alivyovipokea mikononi mwake.
- Katika Sala ya Ekaristi shukrani hutolewa kwa Mungu kwa ajili ya kazi yote ya wokovu; na vipaji vinafanyika Mwili wa Kristo na Damu yake.
- Kwa kuumega mkate na kwa njia ya Komunyo, waamini, ingawa ni wengi, hupokea Mwili wa Bwana kutoka mkate mmoja, na Damu ya Bwana kutoka kikombe kimoja, kama vile mitume walivyopokea kutoka mikono ya Kristo mwenyewe.
- Baada ya Sala ya kuombea Dhabihu, hufuata Sala ya Ekaristi ambapo ndipo kiini chenyewe na kilele cha adhimisho lote kinaanza, yaani Sala yenyewe ya Ekaristi, maana yake; Sala ya kutoa Shukrani na ya kutakatifuza.
Kisha kuhani hualika taifa la Mungu liinue mioyo kwa Bwana kwa sala na kwa kutoa shukrani; na analiunganisha naye kwa sala kuu. Hii ni sala ambayo kwa jina la jumuiya yote, kuhani huielekeza kwa Mungu Baba, kwa njia ya Yesu Kristo katika Roho Mtakatifu. Sababu na maana ya sala hii ndiyo hii: kusanyiko lote la waamini lijiunge na Kristo katika kuyasifu makuu ya Mungu, na katika kumtolea sadaka. Sala ya Ekaristi hudai na kuwataka wote waisikilize kwa heshima na ukimya.
- Ibada-Kanuni ya Komunyo
- Sala ya Bwana
- Ibada - kanuni ya kupeana amani
- Kuumega mkate.
NB: Baada ya taratibu za kupokea Ekaristi kulingana na mwongozo wa Liturjia, kuhani husali Sala baada ya Komunyo. Kwa sala hii kuhani humsihi Mungu atujalie matunda ya fumbo lililoadhimishwa.
Hitimisho la Adhimisho la Misa Takatifu
Ibada ya Adhimisho la Ekaristi Takatifu, humalizika kwa kuhani kutoa Baraka ya Mwisho na maandamano kuelekea Sakristia.
Tukumbuke kuwa; Ibada ya Adhimisho la Misa Takatifu ndiyo kilele cha maadhimisho na ibada zote, hivo hatushauriwi kuendeleza sala au ibada yoyote baada ya kuhitimishwa kwa maadhimisho hayo, ingawa kanisa linaruhusu kwa wale wenye utaratibu mahalia wa pamoja mfano katika seminari zetu ambapo waamini wamelelewa na kukua katika msingi wa utaratibu flani wa sala baada ya Misa.
Makala hii imeandaliwa kwa kunukuu Katekisimu ya kanisa katoliki (KKK), Misale ya Altare, pamoja na Mafundisho ya waalimu wa kanisa.
Tumsifu Yesu Kristo...
Post a Comment