SAKRAMENTI YA UPATANISHO

Kitubio/upatanisho ni sakramenti ya kumwondolea mtu dhambi alizozitenda baada ya ubatizo. Kila mkristo aliyetenda dhambi yampasa kupokea sakramenti ya kitubio kila anapohitaji na kabla ya kupokea sakramenti nyingine

Ibada ya kitubio ina sehemu kuu nne (04), nazo ni;
  • Kutafuta dhambi
  • Kujuta dhambi nakukusudia kuacha dhambi
  • Kuungama dhambi
  • Kutimiza malipizi

A: KUPEKUA/KUTAFUTA DHAMBI MOYONI.

Kabla ya kumwendea padre, tumia wakati fulani na ufikiri moyoni na ujiweke mbele ya Mungu ukifikiri kwanza makosa yako na dhambi ulizozitenda tangu ulipoungama mara ya mwisho. Huwa tunafikiri dhambi kwa;
  • Kupima upendo wetu mbele za Mungu na mahusiano yetu na wenzetu kwamba kama kweli ulizishika na kuziishi amri za Mungu na za Kanisa moja baada ya nyingine bila kusahau hata moja.
  • Kupekua mizizi ya dhambi kama vile, Uasherati, ugomvi, wivu, hasira, fitina, husuda, ulevi uadui, kutokuwa na kiasi n.k
Ukumbuke kuwa dhambi hutendwa kwa mawazo (fikira), kwa maneno, kwa vitendo na pia kwa kutotimiza wajibu


B: KUJUTA NA KUKUSUDIA KUACHA DHAMBI.

Je, ni kwa sababu gani twajuta dhambi zetu?

Twajuta dhambi zetu kwa sababu tumeukosea utatu Mtakatifu na tunastahili adhabu yake na pia bila majuto hatuwezi kupata maondoleo ya dhambi yoyote.

Kumbuka kuwa toba ya kweli huambatana na kujuta dhambi ulizotenda kwa majuto kamili, kwa maana nyingine dhambi hiyo ikuumize moyoni ya kwamba kwanini umeitenda na kwanini unayatonesha madonda ya Yesu kristo msalabani kwa kurudia dhambi alizozifia msalabani kwa ajili ya ukombozi wetu!!, kukusudia kuziacha dhambi hizo na kuepuka nafasi ya kuzitenda kwa kuomba ulinzi na nguvu ya Roho Mtakatifu ili akuongoze kuyashika yale yote yaliyo mema na kuyaacha yaliyo mabaya.

Hivyo basi kabla ya kusogelea sanduku la maungamo au sehemu yoyote kwa ajili ya maungamo yafaa kusali sala hii ya toba;

Ninatubu dhambi zangu zote. Kwa kutenda dhambi nimeshindwa kutimiza yaliyo ya kweli. Nimekukosea na ninaahidi kwamba sitafanya tena na nitafanya kitubio na pia nitaepuka chochote kinachoweza kunirudisha dhambini.

 
C. KUUNGAMA

Unapoingia mahala pa Maungamo sema hivi:

Anayeungama: Tumsifu yesu Kristo Padre.
P. Milele Amina.
Anayeungama: Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu, Amina.

Padre unibariki kwa kuwa nimetenda dhambi

 Padre anamkaribisha anayetaka kuungama kwa maneno Kama haya: "Mungu aliyeng'aa mioyoni mwetu, akuwezeshe kufahamu kweli ubaya wa dhambi zako na huruma yake Mungu."


Mwenye kuungama husema:

Namuungamia Mungu Mwenyezi nawe Padre wangu. Sikuungama tangu ….... (taja mara yako ya mwisho kuungama ilikuwa lini). Niliondolewa dhambi, na nikatimiza malipizi, dhambi zangu ndizo hizi; (Taja dhambi ulizokosa na mara ngapi umezitenda. Usiungame ovyo ovyo tu, bila kutubu, au kama haujanuia kuziacha) na ukumbuke kuwa; Ni bure kuungama bila majuto.

Ukimaliza sema;

Najuta dhambi zangu zote. Ee Yesu, unihurumie. 

au 

Basi padre wangu dhambi zangu ndizo hizi na zile nilizozisahau naomba toba kwa Mungu ili nipate maondoleo ya dhambi.

Sikiliza mafundisho ya Padre, na kuyapokea kwa unyenyekevu. Ukikumbuka kwamba ndiye Yesu Kristo mwenye kukuondolea na kukutakasa kwa maneno ya sakramenti, Padre akisema.


Kisha Padre anamnyoshea mikono miwili au mkono wa kuume tu, yule anayeungama akisema:

Mungu, Baba mwenye huruma, aliupatanisha ulimwengu na nafsi yake kwa kifo na ufufuko wa mwanae; akatushushia Roho Mtakatifu tupate kuondolewa dhambi, Yeye mwenyewe akusamehe na kukupa amani kwa huduma ya kanisa. Nami nakuondolea Dhambi zako kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.

 Anayeungama: Amina.

P. Tumsifu Yesu Kristo.
Anayeungama: Milele Amina.
P. Bwana amekuondolea dhambi zako, nenda na Amani.

 
D.TIMIZA MALIPIZI ULIYOPEWA.

Unaporudi pahali pako, umshukuru Mungu aliyekuondolea dhambi zako, ukumbuke mashauri aliyokupa Padre, ufanye malipizi yako, na kumwomba Mungu akusaidie usifanye dhambi tena.
Ukumbuke tena kusudio lako la pekee. Uzoee kurudia kusudio hilo asubuhi na kujiuliza jioni jinsi ulivyolishika.

Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu Sana, zitakuwa nyeupe kama theluji, zijapokuwa nyekundu kama bendela, zitakuwa kama sufu.' Isaya 1:18


          Tumsifu Yesu Kristo...

Post a Comment

Previous Post Next Post