SALA KILA UNAPOINGIA KANISANI

“Unitakase Ee Bwana mimi, na uovu wangu wote, ili nipate kustahili kushiriki ibada takatifu”, Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina. †
(Sala hii husaliwa ukiwa unachovya maji ya Baraka uingiapo kanisani)

Kisha, upigapo goti kuelekea Tarbenakulo sali;
“Mungu wangu na Bwana wangu. Ninakusifu na kukuabudu katika Ekaristi Takatifu”

 
SALA WAKATI WA KUTOKA KANISANI

“Unilinde Ee Mwenyezi Mungu, nikapate kuwa mfano katika jamii yangu, na nikushuhudie katika matendo yangu” Kwa jina la Bana na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina †
(Sala hii husaliwa unapochovya maji ya baraka wakati wa kutoka kanisani)

 
SALA KABLA YA KUPOKEA EKARISTI TAKATIFU

Ee Yesu Kristo, Mwokozi wangu, katika karamu ya Mwisho, uligeuza mkate kuwa mwili wako, na divai kuwa damu yako, ukawapa mitume, na sasa mapadre uwezo wa kufanya vile vile. Nasadiki kuwa umo kweli katika Ekaristi Takatifu; nitapokea Mwili wako na damu yako, Pamoja na roho yako na Umungu wako. Wewe menyewe ulisema; “Huu ndio mwili wangu”. Ee Yesu, nizidishie Imani.

 
SALA YA KOMUNYO YA KIROHO.

Ee Yesu ninaelekea meza yako takatifu ulimojificha kwa ajili ya kunipenda mimi. Mungu wangu ninakupenda, siwezi kukupokea katika komunyo takatifu, lakini njoo njoo kwangu kwa neema yako. Njoo kiroho moyoni mwangu, utakase moyo wangu, uusafishe moyo wangu uufanye moyo wangu ufanane na wako. Amina.
(Sala hii husaliwa kwa wakristo wakatoliki wasio katika usafi wa Moyo kwa wakati huo; yaani wenye dhambi ya(za) mauti)


SALA KWA MTAKATIFU YOSEFU WA CURPETINO.

Ee Mt. Yoseph wa Curpetino ambaye kwa sala zako ulijaliwa na Mungu katika mitihani yako, neema ya kuulizwa maswali yale tu uliyoyajua; Nisaidie ili niweze kuwa kama wewe kufanikiwa katika mitihani yangu ya (taja mitihani unayoenda kufanya). Naahidi kukufanya ujulikane na watu wamwombe Mungu kupitia wewe.
Ee Mt. Yoseph wa Curpetino, niombee pia niweze kukumbuka yote ninayosoma, nijaliwe pia uwezo wa kujibu kwa usahihi kila swali nitakalotakiwa kulijibu.
Ee Roho Mtakatifu ……………………………… Uniangaze.
Bikira Maria Kikao cha Hekima ……………… Uniombee.
 

SALA KWA MTAKATIFU MIKAELI MALAIKA MKUU.

Mtakatifu Mikaeli Malaika mkuu, utulinde katika vita, uwe kinga yetu katika maovu na maoteo ya shetani, Mungu amtiishe, tunaomba sana, nawe mkuu wa majeshi ya mbinguni kwa nguvu ya Mungu waangushe motoni shetani na pepo wabaya na wengine wote wanao zunguka duniani ili kuzipoteza roho za watu. Amina


SALA YA KUOMBEA MGONJWA

Ee Bwana Yesu Kristu, ulishiriki ubinadamu wetu kwa hiari yako upate kuwaponya wagonjwa na kuwaokoa wanadamu wote. Sikiliza kwa huruma sala zetu, umjalie afya ya mwili na roho huyu ndugu (jina) yetu. Mfariji kwa kinga yako, mpe nafuu kwa nguvu yako. Msaidie atumaini kuokoka kwa njia ya mateso, kama ulivyotufundisha kutumaini hapo ulipoteswa kwa ajili yetu. Utujalie sisi sote amani na furaha zote za ufalme wako huko unakoishi daima na milele. Amina.

 
SALA YA SIKU YA KUZALIWA
Ee Bwana Mungu mwenye upendo, leo ni siku yangu ya kuzaliwa, ninakushukuru kwa kuniwezesha kufikia umri huu mpya. Asante kwa kila pumzi ninayovuta, kwa kila neema na baraka ambazo umenijalia.
Nakushukuru kwa familia yangu, marafiki na wapendwa wangu ambao wananizunguka. Pia nakushukuru kwa kila uzoefu wa furaha na changamoto ambazo umenipa katika mwaka uliopita. Kwa maombezi ya Mtakatifu (Taja Jina la Mtakatifu somo wako) Somo wangu naomba unipe nguvu na hekima ya kukabiliana na changamoto zinazokuja na furaha ya kusherekea mafanikio yangu. Nipe moyo wa shukrani na upendo kwa wengine.
Ee Bwana, niongoze katika mwaka huu mpya wa maisha yangu. Niumegeze na Roho wako Mtakatifu ili niweze kuishi kwa ukaribu nawe, kufuata mapenzi yako na kumtumikia kila mtu ninayekutana nae. Nipe furaha na amani ya ndani, na nipe uwezo wa kutumia vipawa na talanta ulizonipa kwa utukufu wako. Asante tena kwa upendo wako usio na kikomo na neema zako zisizostahiliwa. Natumaini kuwa mwaka huu utakuwa wa baraka na furaha tele. 
Ninaweka maisha yangu mikononi mwako na ninakuomba unipe mwongozo wako katika kila hatua ninayochukua. Ninaomba hayo kwa njia Yesu Kristu Bwana Wetu. Amina


             Tumsifu Yesu Kristo...



Post a Comment

Previous Post Next Post