MAJI YA BARAKA
Maji ya Baraka ni hazina ya kiroho ambayo inaweza kutajwa kama njia ya utajiri wa kiroho. Kwa sababu ya baraka zilizoambatanishwa na maji hayo, Kanisa Takatifu linasisitiza matumizi yake kwa Wanae, hasa katika kipindi cha hatari. Maji ya Baraka ni kisakramenti ambacho hutuondolea dhambi ndogo na yanayo nguvu ya kuchochea sala za Kanisa.
Shetani huyachukia Maji ya Baraka kwa sababu ya nguvu zake dhidi yake, hivyo ni muhimu kuyatumia kwa wingi ili kuwa na nguvu ya kumshinda adui wa roho zetu. Kwa wale walio Toharani, wanajua jinsi roho zao maskini wanavyotamani sana Maji ya Baraka. Kwa hiyo, tunashauriwa kutumia Maji ya Baraka kama njia ya kusafisha roho zetu na kuwa karibu na Mungu.
Je, wafahamu matumizi ya maji ya baraka?
Maji yana umuhimu mkubwa sana katika maisha yetu, hasa katika imani ya Kikristo. Wakristu wa kwanza walitambua uzima na thamani ya maji, na hivyo wakajifunza kuyatumia kwa njia sahihi. Kama vile Tertulliano aliwakumbusha wenzake, hata kama walikuwa wameshaoga kabla ya kusali, bado walipaswa kuosha mikono yao kabla ya maombi. Kwa Klementi wa Alexandria, kunawa mikono kabla ya maombi ilikuwa ishara ya usafi wa ndani. Hii ni sawa na jinsi ambavyo padri anapaswa kuosha mikono yake kabla na baada ya kutayarisha vipaji. Hii ni alama ya usafi wa ndani na heshima kwa Mungu wetu. Kwa hivyo, tunapaswa kuelewa umuhimu wa maji katika maisha yetu na kuyatumia kwa njia sahihi, kama alivyotufundisha Kristo.
Maji ya baraka ni ishara ya uzima na utakaso
Kwa imani ya Kanisa Katoliki, maji yanachukuliwa kuwa ni ishara ya uzima na utakaso. Katika Biblia, maji yamekuwa yakitumika kama ishara ya uzima na utakaso kwa muda mrefu. Kwa mfano, katika Kitabu cha Mwanzo, Roho wa Mungu alikuwa anaangalia juu ya uso wa maji "Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji" (Mwanzo 1:2). Na katika Kitabu cha Zaburi, maji yanatajwa kama chanzo cha uzima "Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa" (Zaburi 1:3).
Katika Agano la Kale, maji yalitumiwa kwa ajili ya utakaso wa watu na vitu. Kwa mfano, Mungu aliwaamuru Waisraeli kuoga kwa maji ili kuwa safi kabla ya kuingia katika tabernakulo " Na Haruni na wanawe wataosha mikono yao na miguu yao humo; hapo waingiapo ndani ya hema ya kukutania; watajiosha majini, ili wasife; au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike, kumteketezea Bwana sadaka ya moto" (Kutoka 30:19-20)
Katika Agano Jipya, maji yalitumiwa kwa kusudi la ubatizo, kama ishara ya kuoshwa kutoka dhambi na kupokea uzima mpya katika Kristo "Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto."(Mathayo 3:11).
Kuhusu gharika kuu, Kitabu cha Mwanzo kinatuambia kuwa Mungu alituma gharika ili kuangamiza waovu wote na kubaki na Nuhu na familia yake tu. Maji yalitumiwa kwa sababu ni ishara ya utakaso na kusafisha na pia kutokana na nguvu zake za kuangamiza. Hii inaonyesha nguvu ya Mungu katika kuangamiza dhambi na kuanzisha upya kwa ulimwengu.
Maji ya baraka ishara ya kuanza utume
Yesu Kristo anabatizwa katika maji kuonyesha ishara ya kuanza utume wake. Katika Mathayo 3:16, tunasoma, "Yesu alipobatizwa, mara akapanda kutoka majini, na tazama, mbingu zikamfungukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake." Hii inaonyesha jinsi maji yanavyohusiana na Roho Mtakatifu na kuanza kwa utume wa Yesu.
Maji ya baraka ni muhimu katika kupata uzima wa kiroho
Katika Yohana 3:5, Yesu alisema, "Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu." Hii inaonyesha jinsi kubatizwa katika maji ni muhimu katika kupata uzima wa kiroho.
Kanisa linatambua umuhimu wa maji kwa kusafisha na kuokoa kutoka dhambini.
Kuna baadhi ya watakatifu ambao wameheshimu maji kama ishara ya uzima wa kiroho, kama vile Mtakatifu Yohane wa Damasko ambaye alisema, "Maji yana nguvu ya kusafisha na kubadilisha, na kwa hivyo yana uwezo wa kutoa uzima wa kiroho."
Wafahamu matumizi ya kiroho ya maji?
- Maji kwa njia ya kristu yamefanywa chombo cha kuzalia watoto wapya wa Mungu kwa ubatizo ili wapate uzima wa milele.
- Kanisa inayapandisha maji kuwa kisakramenti kwa kuyabariki.Kisha hutumiwa kuwabatiza watu,kuwabariki watu na vitu.Pengine maji ya baraka huchanganywa na chumvi.
- Maji ya baraka yatumika kubarikia nyumba ili kuwaimarisha wakazi na kuwafukuza pepo wabaya
- Mara nyingine maji ya baraka yanatumika kunyunyizia watu Dominika kabla ya Misa badala ya kutubu.
Matendo yaletwayo na maji ya baraka
- Kufukuza na kuzuia mashetani.
- Kutoa uzima wa mwili na roho kwa wote wayatumiayo.
- Kuponya magonjwa ya mwili
- Malaika wanazilinda nyumba zile zilizo na maji ya baraka.
- Huleta usalama katika kila hatari.
- Huleta neema za msaada.
- Huzaa watoto wapya kwa ubatizo.
Je! Tuyatumiaje maji ya Baraka
Maji ya Baraka tuyatumie kama ifuatavyo: chovya vidole vyako kwenye maji ya baraka na kisha fanya ishara ya msalaba huku ukisali "Ee Bwana kwa maji haya ya Baraka na kwa Damu Yako Azizi, nitakase dhambi zangu zote". Pia nyunyuzia Roho zilizoko toharani ili uwape tulizo la mateso yao.
HITIMISHO
Maji ya baraka ni ishara ya uzima wa kiroho na yanapaswa kutumiwa kwa kuzingatia umuhimu wake katika imani ya Kanisa Katoliki. Maji yanapaswa kutumiwa kwa kusudi la kusafisha na kuokoa kutoka dhambi na kuanzisha upya uzima wa kiroho.
Tumsifu Yesu kristo...
إرسال تعليق