Je! Wakatoliki wanaabudu sanamu (Msalaba)
Amri ya kwanza ya Mungu inasema"Ndimi Bwana Mungu wako usiabudu Miungu wengine" . Amri hii inatuzuia tusiabudu sanamu, biblia inasema "Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia." (Kut 20:4).
"Jihadharini nafsi zenu basi; maana hamkuona umbo la namna yo yote siku ile Bwana aliyosema nanyi kutoka kati ya moto msije mkajiharibu nafsi zenu, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa sura yo yote, mfano wa mwanamume au mwanamke" (kum 4:15-16)
Maana ndiye Mungu apitaye vitu vyote kabisa aliyejifunua mwenyewe kwa Israeli. "Ndiye vyote" lakini papo hapo, "Ndiye Mkuu juu ya kazi zake." "Yeye aliye asili ya uzuri."
Hata hivyo tangu Agano la Kale, Mungu alipanga au kuruhusu utengenezaji wa sura zilizoonyesha kwa ishara, wokovu kwa njia ya Neno aliyemwilishwa: ndivyo ilivyokuwa na nyoka wa shaba, sanduku la agano na Makerubi.
Mtaguso wa saba wa Nikea (787) ukitegemea fumbo la umwilisho wa Neno, dhidi ya wavunja sanamu, ulithibitisha kuwa halali ibada ya sanamu takatifu ya Yesu, hata ile ya Mama wa Mungu, malaika, na watakatifu wote.
Kwa kumwilishwa, Mwana wa Mungu alianzisha "mpango mpya wa wokovu"
Ibada ya Kikristo ya msalaba si kinyume cha amri ya Kwanza ya Mungu ambayo inakataza kuabudu sanamu. Kwa kweli "heshima inayotolewa kwa msalaba hukifikia kifano cha asili." Na ye yote anayeheshimu msalaba, ndani yake anamheshimu yule ambaye amepigwa chapa juu yake( Yesu kristu)" (Paulines Catechism). Heshima itolewayo kwa sanamu takatifu ni "heshima ya hadhi" na wala si kuabudu ambako ni haki ya Mungu peke yake.
Ibada ya msalaba haituelekezi kwa msalaba wenyewe, kama kitu tu, bali chini ya hali yake wazi kama msalaba ukituongoza kwa Mungu aliyemwilishwa. Mwelekeo kwa msalaba hauishii ndani yake kama sanamu, bali huelekea kwa ukweli ambao msalaba unawakilisha."
Ibada ya kuabudu msalaba ( Veneration Of The Cross )
Katika karne ya saba, Kanisa la Roma lilikubali desturi ya Kuabudu Msalaba kutoka kwa Kanisa la Yerusalemu, ambapo kipande cha mbao kinachoaminika kuwa msalaba wa Bwana kilikuwa kikiabudiwa kila mwaka siku ya Ijumaa Kuu tangu karne ya nne.
Kulingana na mapokeo, sehemu ya Msalaba Mtakatifu iligunduliwa na mama wa mfalme Konstantino, Mtakatifu Helen, katika safari ya kwenda Yerusalemu mwaka wa 326. Simulizi ya karne ya tano inaeleza huduma hii huko Yerusalemu.
Sanduku la fedha lililopakwa dhahabu lenye mbao za msalaba lililetwa mbele. Askofu aliweka masalia juu ya meza katika kanisa la Kusulibiwa na waamini wakakaribia, wakigusa paji la uso na macho na midomo kwenye kuni kama vile kuhani alivyosema (kama vile kila kuhani amefanya tangu wakati huo): 'Tazama, Mbao ya Msalaba.'
Kuabudu au kuheshimu sanamu au uwakilishi wa msalaba wa Kristo haimaanishi kwamba tunaabudu sanamu halisi, bila shaka, bali kile inachowakilisha. Katika kupiga magoti mbele ya msalaba na kuubusu tunatoa heshima kuu kwa msalaba wa Bwana wetu kama chombo cha wokovu wetu. Kwa sababu Msalaba hauwezi kutenganishwa na dhabihu yake, katika kuheshimu Msalaba wake sisi, kwa kweli, tunaabudu Kristo. Hivyo tunathibitisha: 'Tunakuabudu, ee Kristu, na tunakubariki kwa sababu kwa Msalaba wako Mtakatifu Umeukomboa Ulimwengu.'
Mtazamo wa watakatifu Ambrose na Augustino juu ya Mti wa msalaba
walikuwa wakilinganisha mti wa Msalaba na mti wa Edeni. Ulinganisho wao ulikuwa ukitofautisha kati ya mti wa Edeni ulioning’inzwa tunda lililosababisha hukumu yetu, wakati Mti wa msalaba ulining’inizwa tunda ambalo lilituongoza kufikia wokovu wetu. Asili ya mti wa Msalaba na kwa sababu hiyo tunda ambalo hutegemea kutoka kwake ni kiini tofauti kabisa na kile kilichoashiria mwanzoni mwa historia yetu ya kutotii na umbali wetu kutoka kwa Mungu. Kwa sababu hiyo, ikiwa kwa kutotii kwa Adamu wa kwanza, tunda la hukumu yetu lilinyang'anywa kutoka katika mti wa Edeni, na kwa utii wa Adamu mpya tunda la wokovu wetu liling'olewa kutoka mti wa Msalaba, ambalo katika hali ambayo hatuelewi zaidi lakini ya kupendeza na kushangaza inafanana na Adamu mpya huyo huyo, ambaye ni Kristo na ni ndilo tunda. Ni yule ambaye kwa kutii anachukua wokovu ambao unatoka kwa Mungu na kwa hali halisi ni mtu yule yule, yaani Bwana mmoja Yesu Kristu, mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba, tunasali katika (Kanuni ya Imani ya NICEA).
HITIMISHO
Msalaba ni alama ya upendo wa Mungu kwa wanadamu na dhabihu kuu ambayo Yesu aliitoa kwa ajili yetu kwa kufa msalabani. Kupitia kifo na ufufuo wake, Yesu alikomboa wanadamu na kuwapa tumaini la uzima wa milele. Msalaba ni ukumbusho wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwetu sisi wadhambi. Tunaamini kwamba kwa kuchukua misalaba yetu wenyewe na kumfuata Yesu, tunaweza kushiriki katika kazi yake ya ukombozi. Ibada ya msalaba haionyeshi ibada kwa sanamu bali ni heshima kwa msalaba wa Bwana wetu kama chombo cha wokovu wetu. Kwa hiyo, tunaabudu na kufanya ishara ya msalaba kama njia ya kuonyesha heshima kwa Mungu na kumfuata Yesu. Msalaba ni alama ya upendo, matumaini na wokovu wetu.
Tumsifu Yesu kristu.....
إرسال تعليق