DHAMBI

Dhambi, ni kuvunja kwa makusudi au bahati mbaya Amri za Mungu, au sheria za kanisa. Mtume Yohana anasema kila lisilo haki ni dhambi. (rejea 1 Yoh 5:17). Kuvunja kwa makusudi ni pale mtu anafahamu lililo jema na anaamua kutotenda, (Yak 4:17 “basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi.”) hivo tunaweza kusema sasa kuwa, Dhambi ni kujua mapenzi ya Mwenyezi Mungu, nini anataka na tunaamua kutimiza kwa kadri ya mapenzi au matamanio yetu.

 

Je, Dhambi zaweza kugawanya katika makundi gani?

   Sote twafahamu ya kuwa kila dhambi, ni uasi (1 Yoh 3:4). Na mshahara wake kwa uasi wowote ule ni mauti. Lakini dhambi zote si sawa, kwa maana ya kwamba dhambi hutofautiana adhabu kulingana na namna kosa lilivyotendeka. Rejea (Lk 12:47-48)“Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana. Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.” Pia rejea maandiko yafuatayo; (Mt 23:14 na Yn 19:14)  

Imeandikwa; (1 Yoh 5:16)“Mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti. Iko dhambi iliyo ya mauti. Sisemi ya kwamba ataomba kwa ajili ya hiyo. Kila lisilo la haki ni dhambi, na iko isiyo ya mauti”. Hivyo ipo dhambi iliyo ya mauti, dhambi isiyo ya Mauti. (na zaidi ipo dhambi ya Kumkufuru Roho mtakatifu.) Kwa kadri ya katekisimu ya kanisa katoliki, dhambi za mauti ndiyo inayojulikana kama dhambi kubwa au nzito, na dhambi isiyo ya mauti ndiyo inayojulikana kama dhambi ndogo au nyepesi.

 

DHAMBI YA MAUTI

Je, dhambi za mauti ni zipi?

   Ili dhambi iwe ya mauti, kwanza; iwe kubwa na umeitenda kwa makusudi, yaani umekusudia kutenda ukiwa na utimamu pili; tukiwa na maarifa kamili, kuwa unachoenda kukitenda ni kinyume na sheria ya Mungu inavyotuongoza na tatu; kwa hiari yako wenyewe tunaamua kufanya kwa kadri ya sisi tunavyotaka na kupuuza maagizo yake Mwenyezi Mungu.

 

Je, kwanini huitwa dhambi za mauti, na matokeo yake ni nini?

   Ndugu zangu, dhambi hizi huitwa dhambi za mauti (sins unto death) kwa sababu mtu akizifanya aweza kweli kusamehewa na kuingia katika ufalme wa mbinguni, lakini adhabu ya kifo hapa duniani haikwepeki kwake. Hivo yeyote afanyaye dhambi kama hizi roho yake yaweza urithi ufalme wa mbingu endapo atatubu, lakini mauti haina budi kumpata. Basi kama matokeo; hubeba adhabu ya milele yaani, ni dhambi zinazotutenganisha na Mungu, kwa sababu kupitia hizo tunamkataa Mungu, tunampa kisogo; kwa maneno mengine, kwa kupitia dhambi tunamwambia kwamba hatutaki kuwa na uhusiano wowote naye.

 

Je, kuna mifano gani katika biblia inayoonesha maonyo na adhabu juu ya dhambi ya mauti?

   Mfano wa watu waliofanya dhambi kama hizi katika biblia walikuwa ni  Wana wa Israeli. Utaona japokuwa walitendewa mambo mengi na miujiza Mingi na Mungu lakini, hawakumcha yeye, kinyume chake, wakaendelea kuwa wanung’unikaji, wazinzi, na waabudu sanamu, Hivyo ikafika wakati Mungu akaghairi kutembea nao, akaapa kuwa hakuna hata mmoja wao atakayeiona hiyo nchi ya Ahadi. Wote watakufa jangwani. Na kweli japokuwa walilia na kuomboleza na kutubu sana, lakini Mungu hakusikia kilio chao wote, walikufa wote jangwani.

(1 Kor 10:1-12) “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze. Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu. Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka. Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu. Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke”.

 Ipo mifano mingi sana ya dhambi kama hizi katika biblia, Ukisoma agano jipya. Utaona mitume walitoa maagizo kwa kanisa juu ya watu wanaotenda dhambi za uzinzi, wakabidhiwe shetani ili mwili uangamie lakini roho zao zipone katika siku ile ya Bwana…

Tukirejea (1Kor 5:1-13) “Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye. Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo. Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo. Katika jina la Bwana wetu Yesu, ninyi mkiwa mmekusanyika pamoja na roho yangu, pamoja na uweza wa Bwana wetu Yesu; kumtolea Shetani mtu huyo, ili mwili uadhibiwe, ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana Yesu”.

 

Je, tufanye nini tunapoanguka katika dhambi ya mauti?

   Kwa kugundua kuwa tumemkosea Mwenyezi Mungu na tumejitenga naye, tupaswa kwenda kufanya toba kwa Mungu kupitia sakramenti ya upatanisho. (Hivo kama mkristo Mkatoliki mtafute Padre au Askofu na uungame dhambi zako). Tukumbuke kuwa hatupaswi kupokea Ekaristi Takatifu tukiwa na dhambi ya mauti kwani ni kufuru na ni kosa kubwa sana linalofanyika juu ya sakramenti ya mwili na damu ya BWANA wetu Yesu Kristo.

 

DHAMBI ISIYO YA MAUTI

Je, dhambi nyepesi au isiyo ya mauti ni ipi?

Hizi ni dhambi ambazo mtu hutenda bila ya kuwa na maarifa kamili ya kile anachokitenda, hutokea amevunja sheria kwa bahati mbaya au bila makusudio au idhini (hiari) yake. Mtu akitenda aweza kusamehewa kwa Mungu kwa njia ya sakramenti ya upatanisho bila ya adhabu yoyote, na hata akipokea adhabu basi haitakuwa adhabu ya kumfanya umauti umpate.

Dhambi nyingi tunazozitenda leo hii zinaangukia katika kundi hili. Pale mtu anapotubu kwa kumaanisha Mungu anamsamehe, aidha kwa adhabu kidogo au bila adhabu kabisa, kwa mfano Petro alipomkana Bwana, alikwenda kutubu na akasamehewa, bila hata ya adhabu yoyote. (1 Yohana 5:16) “Mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti. Iko dhambi iliyo ya mauti. Sisemi ya kwamba ataomba kwa ajili ya hiyo. Kila lisilo la haki ni dhambi, na dhambi iko isiyo ya mauti.”

 

Uhusiano kati ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na dhambi zisizo za mauti.

   Tukumbuke kwamba dhambi nyepesi au isiyo ya mauti hupunguza uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu kwani bado tu, washirika naye lakini kwa kiwango pungufu ya kile cha mwanzo. Hivo kwa Imani na nguvu ya Ekaristi Takatifu, tunampokea Kristo anayetupatia nguvu kwa kuishi ndani yetu ili tuweze kuepuka dhambi na vishawishi naye aweze kutenda ndani yetu. Hivo Ekaristi Takatifu hutuneemesha kwa kutupatia hofu ya kutomkosea Mwenyezi Mungu na huweza kurudisha uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu, lakini sio kuondoa dhambi; Hivo basi Ekaristi Takatifu inarudisha uhusiano wetu lakini adhabu inabaki palepale ambapo kwa dhambi zisizo za mauti adhabu huondolewa kupitia Sakramenti ya upatanisho. (Ebr 4:16) “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

 

DHAMBI YA KUMKUFURU ROHO MTAKATIFU

Je, mtu anamkufuru vipi Roho Mtakatifu mpaka kupeleke asisamehewe kabisa?

   Dhambi hii Bwana Yesu aliinena kutokana na tabia aliyoiona kwa wale mafarisayo na waandishi waliokuwa wamemzunguka. Walikuwa ni watu wanaoishi maisha ya unafiki wakijua ukweli lakini wasiutende na kibaya zaidi waliutumia ujuzi wao kuwapotosha hata na wengine wasiufahamu ukweli, na ndio maana Bwana Yesu aliwakemea sana.

Tukirejea (Mathayo 23). Katika kisa hiki walimwona Bwana akitoa pepo kwa uweza wa Roho wa Mungu, Na hilo walilifahamu kabisa. Na ndio maana yule farisayo mmoja aliyeitwa Nikodemo aliyemfuata usiku na kumwambia Rabi “TWAJUA” kuwa umetoka kwa Mungu rejea (Yn 3:1-2), Ikiwa na maana kumbe mafarisayo wote walijua ukweli lakini kwa sababu ya wivu wakaanza kumzushia Bwana uongo kuwa Roho iliyo ndani yake ni ya Beelzebuli na si ya Mungu  ili tu watu wasimwamini. Na kwa sababu hiyo basi wakawa wameshaitenda dhambi hii ya kumkufuru Roho Mtakatifu.

 

(Mt. 12:22-32)Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona. Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yoyote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje? Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu. Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu?. Ndipo atakapoiteka nyumba yake. Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya. Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa. Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao.”

Hii ni kutufundisha kuwa tuwe makini na kazi za Roho Mtakatifu..mahali ambapo nguvu za Mungu za kweli zinaonekana, injili ya kweli inahubiriwa, Roho Mtakatifu anatenda kazi halafu tunatoa maneno ya kukebehi au kudhihaki, kusema; Zile ni nguvu za giza kwa wivu tu, basi tupo hatarini kuitenda dhambi hii.

Hivyo kwa kuhitimisha, dhambi hii hutendwa kwa watu waufahamuo ukweli lakini kwa makusudi wanaupinga kwa faida zao wenyewe. lakini si kwa mtu ambaye hana maarifa, kwasababu wengine wanakufuru kwa ujinga wao tu. Hawa wanasamehewa. Vilevile mawazo mabaya kinyume na Roho Mtakatifu hayakufanyi uwe umemkufuru Roho Mtakatifu. Ukiona kuna vitisho ndani yako kwamba umemkufuru Roho Mtakatifu vikatae huo ni uongo wa shetani. Wanaomkufuru Roho Mtakatifu hofu ya Mungu huwa haipo ndani yao hata kidogo, na ndio maana wanayafanya hayo hadharani.

 

Tumsifu Yesu kristo...

 

 

Post a Comment

أحدث أقدم