MASOMO YA MISA, FEBRUARI 5, 2024
JUMATATU YA MWAKA 


SOMO 1
1Fal 8:1-7,9-13

Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila, wakuu wa mbari za mababa wa wana wa Israeli, wamwendee mfalme Sulemani huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la agano la Bwana kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni. Wakakutana mbele ya mfalme Sulemani watu wote wa Israeli wakati wa sikukuu, katika mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba. Wazee wote wa Israeli wakaja, nao makuhani wakajitwika sanduku. Wakalipandisha sanduku la Bwana, na ile hema ya kukutania, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa katika ile Hema; vitu hivyo makuhani na Walawi wakavipandisha. Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli waliokutanika kwake, walikuwako pamoja naye mbele ya sanduku, wakichinja sadaka kondoo na ng'ombe, wasioweza kuhesabiwa wala kufahamiwa idadi yao kwa kuwa wengi. Makuhani wakalileta sanduku la agano la Bwana hata mahali pake, katika chumba cha ndani cha ile nyumba, patakatifu pa patakatifu, naam, chini ya mbawa za makerubi. Kwa maana makerubi yalinyosha mbawa zao, juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu.Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, Bwana alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri. Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya Bwana ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya Bwana ilikuwa imejaa utukufu wa Bwana. Ndipo Sulemani akanena, Bwana alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab 132:6-10

(K) Ee Bwana,uinuke, uende kwenye raha yako

Tazama, tulisikia habari zake katika Efrata,
Katika konde la Yearimu tuliiona.
Na tuingie katika maskani yake,
Tusujudu penye kiti cha kuwekea miguu yake.

Ee Bwana, uinuke, uende kwenye raha yako,
Wewe na sanduku la nguvu zako.
Makuhani wako na wavikwe haki,
Watauwa wako na washangilie.
Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako,
Usiurudishe nyuma uso wa masihi
(K) Ee Bwana,uinuke, uende kwenye raha yako.


SOMO 2
1 Kor. 15:1-11

Ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri; isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapa mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake. Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami. Basi, kama ni mimi, kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


SHANGILIO
Mt. 8:17

Aleluya, aleluya,
Aliutwaa udahifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu.
Aleluya.


INJILI
Mk 6:53-56

Yesu na wanafunzi wake walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. Nao wakiisha kutoka mashuani, mara watu walimtambua, wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi, kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo. Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Post a Comment

أحدث أقدم