MASOMO YA MISA, JANUARI 24, 2025

IJUMAA, JUMA LA 2 LA MWAKA WA KANISA

KUMBUKUMBU YA MT. FRANSISKO WA SALES (ASKOFU NA MWALIMU WA KANISA)


SOMO 1
Ebr. 8:6 – 13

Kuhani wetu sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora. Maana kama lile la kwanza lingalikuwa halina upungufu, nafasi isingalitafutwa kwa lile la pili. Maana, awalaumupo, asema, Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nami nitawatimizia nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda agano jipya; halitakuwa kama agano lile nililoagana na baba zao, katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri. Kwa sababu hawakudumu katika agano langu, Mimi nami sikuwajali, asema Bwana.

Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli baada ya siku zile asema Bwana; nitawapa sheria zangu katika nia zao, na katika mioyo yao nitaziandika; nami nitakuwa Mungu kwao, nao watakuwa watu wangu. Nao hawatafundishana kila mtu na jirani yake, na kila mtu na ndugu yake, akisema, Mjue Bwana; kwa maana wote watanijua, tangu mdogo wao hata mkubwa wao. Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, na dhambi zao sitazikumbuka tena. Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 85:7, 9 – 13 (K)

(K) Fadhili na kweli zimekutana.

Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako,
Utupe wokovu wako.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu. (K)

Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na Amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)

Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)



SHANGILIO
Efe. 1:17, 18

Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya.



INJILI
Mk. 3:13-19

Yesu alipanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo. Akawaweka wale Thenashara; na Simoni akampa jina la Petro; na Yakobo, mwana wa Zebedayo, na Yohane nduguye Yakobo, akawapa jina la Boanerge, maana yake, wana wa ngurumo; na Andrea, na Filipo, na Bartholomayo, na Mathayo, na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Thadayo, na Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyemsaliti.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Post a Comment

أحدث أقدم