MASOMO YA MISA, JANUARI 30, 2025 ALHAMISI, JUMA LA 3 LA MWAKA SOMO 1 Ebr. 10:19 – 25 Ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu; na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa Imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya; tumeoshwa miili kwa maji safi. Na tulishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu; tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi iya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia. Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu. WIMBO WA KATIKATI Zab. 24:1 – 6 (K) 6 (K) Hiki ndicho kizazi cha wautafutao uso wako, Ee Bwana. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake. Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari, Na juu ya miti ya maji aliithibitisha. (K) Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake? Mtu aliye na moyo safi na moyo mweupe Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili, Wala hakuapa kwa hila. (K) Atapokea Baraka kwa Bwana, Na haki kwa Mungu wa wokovu wake. Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao, Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K) SHANGILIO 1Pet. 1:25 Aleluya, aleluya, Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu. Aleluya. INJILI Mk. 4:21-25 Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango? Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi. Mtu akiwa na masikio ya kusikia, na asikie. Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa. Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo

Post a Comment

أحدث أقدم