Somo la Kwanza
Ezra 6: 7 - 8, 12b, 14 - 20
Siku zile: Dario mfalme aliwaandikia magavana wa jimbo la Ng'ambo ya mto, akisema, "Mwacheni gavana wa Wayahudi na wazee waendeleze ujenzi wa nyumba ya Mungu; na wapajenge upya mahali pale pa awali. Ninatoa pia amri hii juu ya kushughulika kwenu na wazee hao wa Kiyahudi katika kuijenga upya tena hiyo nyumba ya Mungu: kutoka hazina ya kifalme yaani kodi za ng'ambo ya Eufrete Magharibi, gharama za watu hao zilipwe kikamilifu, bila kukawia ili kazi isikwame. Mimi, Dario, nimetoa amri hii, lazima itimizwe kikamilifu." Nao wazee wa Kiyahudi wakitiwa moyo na mahubiri ya manabii Hagai na Zakaria, mwana wa Ido, walifanya maendeleo ya haraka katika ujenzi. Walifanikiwa kumaliza ujenzi kadiri ya amri ya Mungu wa Israeli na amri za wafalme Sairusi, Dario na Artashasta, mfalme wa Uajemi. Hekalu lile lilikamilika kujengwa siku tatu ya mwezi Adari, katika mwaka wa sita wa utawala wa mfalme Dario. Wana wa Israeli - makuhani, Walawi, na watu wengine waliopanda kutoka uhamishoni - waliadhimisha kwa shangwe kuwekwa wakfu kwa hekalu la Mungu. Kwa kuwekwa wakfu kwa hekalu hili la Mungu, walitoa sadaka fahali mia, kondoo dume kumi na wawili kuwa sadaka ya dhambi kwa Waisraeli wote, kadiri ya hesabu ya makabila kumi na mawili ya Israeli. Baadaye wakawaweka makuhani kwa vyeo vyao na Walawi kadiri ya zamu zao za utumishi wa ibada ya Mungu kule Yerusalemu, kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Musa. Hawa waliorudi kutoka uhamishoni, waliiadhimisha Pasaka katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. Walawi ambao kila mmoja alijitakasa kwa ajili ya tukio hilo, walifanya matoleo ya sadaka za Pasaka kwa ajili ya watu wote waliotoka uhamishoni, kwa ajili ya ndugu zao makuhani, na kwa ajili yao wenyewe.
Neno la Bwana, Tumshukuru Mungu.
Zaburi
Zaburi 122: 1 - 2, 3 - 4a, 4b
Nalifurahi waliponiambia,
twendeni nyumbani kwa Bwana.
Sasa miguu yetu imesimama
ndani ya malango yako, ee Yerusalemu. K.
Yerusalemu uliojengwa
kama mji ulioshikamana.
Ndiko wanakopanda makabila,
makabila ya Bwana. K.
Kama ilivyo sheria ya Israeli,
ili walitukuze jina la Bwana.
Humo vimewekwa viti vya hukumu,
viti vya nyumba ya Daudi. K.
Shangilio
Luka 11: 28
Aleluya, Aleluya
Wana heri wenye kulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya.
Injili
Luk 8: 19 - 21
Wakati ule: Mama yake na ndugu zake walikwenda kumtazama Yesu, lakini walishindwa kuonana naye kwa sababu ya umati wa watu. Akapashwa habari, "Mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kuonana nawe." Akawajibu akisema, "Mama yangu na ndugu zangu ndio wenye kulisikia neno la Mungu na kulifuata"
Neno la Bwana, Sifa Kwako Ee Kristo.
إرسال تعليق