Maisha ya Watakatifu Andrew Kim Taegon, Paul Chong Hasang na Wenzake
Mtakatifu Andrew Kim Taegon (21 Agosti 1821 – 16 Septemba 1846) alikuwa padri wa kwanza mzawa wa Korea na mtoto wa wazazi waliokuwa Wakristo wapya. Baada ya kubatizwa akiwa na umri wa miaka 15, alisafiri maili 1,300 kwenda kusomea seminari huko Macao, China. Baada ya miaka sita alifanikiwa kurudi Korea kupitia Manchuria. Mwaka huo huo alivuka Bahari ya Njano hadi Shanghai ambako alipewa daraja la upadri. Aliporudi nyumbani, alipewa jukumu la kupanga njia ya kuingiza wamisionari kwa njia ya maji ili kuepuka walinzi wa mipaka. Hata hivyo, alikamatwa, akateswa na hatimaye akachinjwa karibu na Mto Han, Seoul.
Baba yake Andrew, Ignatius Kim, aliuawa shahidi wakati wa mateso ya mwaka 1839 na alitangazwa mwenye heri mwaka 1925. Paul Chong Hasang, mtume mlei na mtu wa ndoa, naye pia alikufa shahidi mwaka huo huo akiwa na umri wa miaka 45.
Miongoni mwa mashahidi wengine wa mwaka 1839 alikuwa Columba Kim, mwanamke asiye na ndoa mwenye umri wa miaka 26. Aliwekwa gerezani, akachomwa na vyuma moto na makaa yanayowaka. Yeye na dada yake Agnes walivuliwa nguo na kuwekwa siku mbili gerezani na wafungwa wa kifo, lakini hawakudhulumiwa. Baada ya Columba kulalamikia udhalilishaji huo, wanawake wengine hawakuteswa tena kwa namna hiyo. Hatimaye walikatwa vichwa.
Mtoto Peter Ryou, mwenye umri wa miaka 13, aliteswa vibaya kiasi cha ngozi yake kung’oka na kuirusha kwa majaji wake. Aliuawa kwa kunyongewa. Protase Chong, mwenye umri wa miaka 41, alikana imani yake chini ya mateso na akaachiwa huru, lakini baadaye alirudi, akaungama imani yake na kuteswa hadi kufa.
Historia ya Kanisa Korea
Ukristo uliletwa Korea wakati wa uvamizi wa Kijapani mwaka 1592, baadhi ya Wakorea walipobatizwa na askari Wakristo kutoka Japani. Injili ilienea kwa shida kwa kuwa Korea ilijifungia dhidi ya dunia ya nje isipokuwa kutuma kodi Beijing kila mwaka. Katika moja ya safari hizo, mnamo 1777, Wakorea walipata vitabu vya Kikristo kutoka kwa Wajesuiti wa China na kuanza kusoma. Kanisa la nyumbani likaanzishwa. Miaka 12 baadaye, padri Mchina aliingia kwa siri na akakuta Wakristo 4,000, hakuna hata mmoja aliyewahi kumuona padri. Baada ya miaka saba walikuwa tayari 10,000. Uhuru wa kidini ulipatikana Korea mwaka 1883.
Papa Yohane Paulo II, alipozuru Korea mwaka 1984, aliwatangaza watakatifu Andrew Kim, Paul Chong na mashahidi wengine 101, wakiwemo maaskofu, mapadri na hasa waumini wengiwengi wa kawaida—wanawake 47 na wanaume 45—waliouawa kwa ajili ya imani kati ya mwaka 1839 na 1867.
Tafakari
Tunastaajabu jinsi Kanisa la Korea lilivyoweza kusimama kwa miaka mingi likiwa Kanisa la waumini bila mapadri. Waliendeleaje bila Ekaristi? Hii inatufundisha kuwa kabla ya sakramenti kuna haja ya imani hai. Sakramenti ni alama za hatua ya Mungu kujibu imani iliyo tayari kuwepo. Zinakua na kuimarisha neema na imani, lakini tu ikiwa kuna kitu cha msingi cha kukuzwa.
WATAKATIFU ANDREW KIM TAEGON, PAUL CHONG HASANG NA WENZAKE, MTUOMBEE..
إرسال تعليق