Sikukuu hii ilianzishwa kutokana na madhulumu yaliyofanywa na Waislamu waliovamia bara la Ulaya, hususan nchi za Italia, Hispania, Ugiriki na Ufaransa. Wakristo waliteswa kwa ajili ya imani yao na wengi wakachukuliwa mateka. Licha ya mateso hayo, walibaki imara katika imani.
Mnamo mwaka 1220, kijana mmoja Mfaransa aitwaye Petro Nolasko aliguswa sana na mateso hayo, akatafakari namna ya kuwakomboa wakristo waliokuwa mateka. Akiwa pamoja na Padre Raymond Penyafort na Mfalme Yakobo wa Kwanza wa Aragoni nchini Hispania, waliandaa kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ukombozi wa Wakristo.
Petro Nolasko na wenzake walikumbuka maneno ya Kristo: “Pasipo mimi hamwezi kufanya jambo lolote” (Yohane 15:5). Hivyo walijikabidhi chini ya ulinzi wa Bikira Maria kwa kuanzisha Shirika la Bikira Maria Mama wa Huruma. Kazi ya ukombozi wa Wakristo ilifanikiwa kwa msaada na maombezi ya Mama Maria.
Maria, kwa namna ya pekee, ameshiriki karibu kabisa katika kazi ya ukombozi wa wanadamu, na hachoki kutuombea. Tumkimbilie daima, kwani yeye ni Mama mwenye huruma na anatambua shida zetu. Mfano mzuri tunaona kule Kana ya Galilaya, alipogundua wanaharusi wameishiwa divai, akamwendea mwanawe Yesu (Yohane 2:1-11).
Vivyo hivyo, hata sasa akiwa mbinguni haachi kutuhurumia. Ndiyo maana amejitokeza mara nyingi kwa wanadamu katika maeneo mbalimbali: Fatima, Ureno; Lurdi na La Salette, Ufaransa; na Kibeho, Rwanda. Katika matukio haya yote Mama Maria alitoa ujumbe, hasa wa toba na uongofu. Huu ni ushahidi wa wazi kuwa yeye ni Mama wa huruma.
Tumkimbilie daima, atusaidie kudumu imara katika imani yetu, tuiishi na kuishuhudia.
BIKIRA MARIA MAMA WA HURUMA, UTUOMBEE..
إرسال تعليق