FADHILA
Fadhila ni tunda la mazoea ya kutenda mema. Ni tabia ya kawaida na imara inayomruhusu mtu si kutenda mema tu, bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mt. Gregory wa Nyasa alisema; "Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu."
"... yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya staha, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo." Wafilipi 4:8
Je, kuna aina ngapi za fadhila?
Kulingana na mapokeo ya kanisa katoliki, zipo aina kuu mbili za fadhila, nazo ni; Fadhila za kibinadamu na Fadhila za kimungu.
- Fadhila za Kibinadamu
Fadhila kuu za kibinadamu zipo nne (04) nazo ni; Busara, haki, nguvu na kiasi.
Busara: Hii ni fadhila inayoiandaa akili ya kawaida kupambanua katika mazingira yote mema na ya kweli, na kuchagua njia zitakiwazo kuyapata. Mithali 14:15 "Mtu mwenye busara huangalia sana aendavyo." 1Pet 4:7 "iweni na akili, mkeshe katika sala". Busara haichangamani na hofu au woga, wala hila au udanganyifu, nayo huongoza hukumu ya dhamiri ya mtu. Hivyo kwa msaada wa fadhila hii, Mwenyezi Mungu anatuhitaji sote kuwa watakatifu wenye akili na busara, kwa sababu bila busara ni rahisi kutembea katika njia mbaya. rejea Mt 10:16
Haki: Hii ni fadhila iliyo na utashi thabiti wa kumpa Mungu na jirani iliyo haki yao. mtu mwenye haki hutofautishwa kwa unyoofu wa mwenendo wake kwa jirani. Law 19:15 "usimpendelee mtu maskini, wala kumstaajania mwenye nguvu; baliutamhukumu jirani yako kwa haki." vilevile tunaona; Kol 4:1 "Ninyi akina bwana, wapeni watumwa wenu yaliyo haki, na adili, mkijua kuwa ninyi nanyi mna Bwana mbinguni."
Nguvu: Hii ni fadhila inayothibitisha ushupavu katika magumu na uthabiti katika kufuata mema. Fadhila humwezesha mkristo kushinda hofu, hata hofu ya kifo, na kukabiliana na majaribu, na madhulumu. Katika yote tunayopitia tutembee na mstari usema "Bwana ni nguvu yangu na wimbo wangu." rejea Zab 118:14. Kristo pia anazidi kutuimarisha katika fadhila hii na kwa yoyote yale tunayopitia akisema; "Ulimwenguni mnayo dhiki, lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu" Yoh 16:13
Kiasi: Hii ni fadhila inayoratibu mvuto wa furaha na hutoa usawa katika kutumia viumbe. Maandiko matakatifu yanatukumbusha kutoambatanisha roho zetu pamoja tamaa za mioyo yetu. Ybs 5:2, bali tunaaswa kuishi kwa kiasi, na haki na utauwa katika maisha yetu ya kila siku.
- Fadhila za Kimungu
Kwa imani; twamsadiki Mungu na twasadiki kila kitu alichotufunulia na kile Kanisa Takatifu linachosema ni cha kusadiki. Kwa matumaini; twaamini na kwa tumaini imara twangojea toka kwa Mungu uzima wa milele na neema za kutustahilia uzima huo. na zaidi, Kwa mapendo; twampenda Mungu kuliko vitu vyote na jirani yetu kama tunavyojipenda wenyewe kwa ajili ya Mungu.
Hivyo basi, kama wakristo, tunahimizwa kujijenga katika fadhila hizo za kibinadamu (busara, haki, nguvu na kiasi) ili zitusaidie katika maisha yetu ya kila siku na kumwomba Mungu atujalie fadhila za Kimungu (imani, tumaini na upendo), kwani kwa kufanya hivyo ndivyo tunavyojengeka katika utakatifu na kumtukuza Mungu kupitia matendo yetu.
Amani na salama...
إرسال تعليق