Somo la Kwanza
Rum 15:14-21
Ndugu zangu, nimehakikishwa mimi
mwenyewe kwa habari zenu ya kuwa ninyi nanyi mmejaa wema, mmejazwa elimu yote,
tena mwaweza kuonyana. Lakini nawaandikia, kwa ujasiri zaidi katika sehemu za
waraka huu, kana kwamba kuwakumbusha, kwa neema ile niliyopewa na Mungu, ili
niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu
kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na
Roho Mtakatifu. Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu mbele za
Mungu. Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu,
Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo, kwa nguvu za ishara na maajabu,
katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata ikawa tangu Yerusalemu, na kando kando
yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu;
kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo
limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine; bali kama
ilivyoandikwa, Wale wasiohubiriwa habari zake wataona, Na wale wasiojasikia
watafahamu.
Neno la Bwana, Tumshukuru Mungu.
Wimbo wa Katikati
Zab 98:1-4
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki
yake.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa
Mungu wetu.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni
zaburi.
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
Somo la Injili
Lk 16:1-8
Yesu aliwaambia wanafunzi wake,
Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu alishitakiwa
kwake kuwa anatapanya mali zake. Akamwita, akamwambia, Ni habari gani hii
ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili
tena. Yule wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu
ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya. Najua nitakalotenda,
ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao. Akawaita wadeni
wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu?
Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika
hamsini. Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani? Akasema, Makanda mia ya
ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini. Yule bwana akamsifu wakili
dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika
kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru.
Neno la Bwana, Sifa kwako Ee Kristo.

Post a Comment