Maisha ya Mtakatifu Wilibrodi, Askofu na Mtawa

Wilibrodi, mtume wa Uholanzi, alizaliwa Uingereza mwaka 658. Alipokuwa na umri wa miaka saba, wazazi wake walimpeleka shuleni katika Monasteri, ili akasomeshwe.

Toka hapo aliingia utawani na kwa uongozi wa walimu wenye akili aliendelea katika maarifa ya dini kadhalika na katika maarifa mengine.

Alipokuwa na umri wa miaka thelathini, alipadrishwa, akavuka bahari kwenda kuhubiri Injili kwa watu wa Uholanzi.

Alijaliwa kuwaongoa watu wengi wakawa Wakristo katika dini Katoliki, akajenga Kanisa mjini Utrekt. Baadaye, alisafiri Roma na huko alipata Uaskofu kwa mikono ya Papa.

Akarudi Utrekt, ambako alijenga Kanisa.

Baadaye, akaanzisha Monasteri mjini Echternach (Luksemburg), ambayo ndiyo yakawa makao yake na kitovu cha utendaji wa shughuli zake.

Toka hapa akaelekea tena Kaskazini kuzieneza shughuli zake mkoani Friesland (Uholanzi). Akaenda Kaskazini zaidi ili kuhubiri nchini Denmark, lakini hakufanikiwa.

Katika safari yake ya kurudi toka nchi hiyo, dhoruba ilimchukua, ikampeperusha hadi kisiwa cha Heligoland.

Kwa maoni ya wakazi wake, kisiwa hiki kilikuwa mahali patakatifu na kwa hiyo walidhani ni lazima kabisa kuulinda ukimya kila walapo, wanywapo kwenye chemchemi au kuchinja mnyama. Wilibrodi akataka kuwasadikisha watu kwamba maoni yao yalikuwa potovu.

Basi, akabatiza watu watatu kwenye chemchemi yao, akachinja ng'ombe kwa ajili ya sikukuu.

Muda wote alipokuwa anafanya hayo, alikuwa anazungumza kwa sauti.

Wenyeji walikuwa na hakika kwamba Wilibrodi na wenzake watarukwa na akili, lakini wapi! Walipowaona kuwa ni wazima kabisa, walikasirika sana na kujiuliza kama labda miungu wao walikuwa hawana nguvu tena; baadhi yao walisema kwamba miungu yao ilikuwa na uvumilivu mwingi sana.

Mfalme alipoarifiwa habari za matukio hayo, akaamuru Mmisionari mmoja auawe.

Basi, mmoja wa waandani wake Wilibrodi, akamfia Bwana Yesu.

Kutoka kisiwa cha Heligoland akarudi Uholanzi, akateremkia kisiwa cha Walkeren. Hapo upendo na uvumilivu wake uliwavutia wengi kwenye dini ya Kikristo, lakini Wilibrodi alipoiangusha sanamu iliyoangaliwa na wenyeji kama Mungu wao, kasisi wake akakasirika sana na kujaribu kumwua Wilibrodi. Huyo akafaulu kujiokoa, akarudi salama Utrekt.

Dini ya Kikristo ilienea kwa taratibu katika sehemu nyingi za Uholanzi, Mwenendo wa wenyeji wa mkoa wa Friesland ambao wakati ule walikuwa bado wakali na wakorofi, ulibadilika polepole.

Mtakatifu Wilibrodi alifariki dunia katika Monasteri yake kule Echternach (Luksemburg), mnamo Novemba 7, 739.

Alikuwa mzee mwenye umri wa miaka themanini na moja.

Hati, aliyoiandika yeye mwenyewe, ipo bado imehifadhiwa mjini Paris (Ufaransa).

Ndani ya hati hiyo aliandika kwamba alivuka Bahari ya Kaskazini mwaka 690 na kwamba aliwekwa wakfu kuwa Askofu mjini Roma mwaka 695.


MTAKATIFU WILIBRODI, UTUOMBEE..

Post a Comment

Previous Post Next Post