MAISHA YA MWENYEHERI YOHANA MARIA MAYE, NOVEMBA 6

Mama huyo alizaliwa Ufaransa mnamo mwaka 1331 katika jamaa ya watu wenye cheo.

Alikuwa mtoto aliyependa sana kusali.

Siku moja sala zake zilimwokoa mtoto wa kiume aliyekuwa ametumbukia katika bwawa la maji mengi.

Mtoto huyo aliitwa jina lake Roberto wa Sile.

Huyo alipokua, alimpenda Yohana, na baada ya miaka kadhaa babu yake Yohana alifanya mpango wapate kufunga ndoa.

Tangu utoto wake, Yohana alikuwa na nia ya kujitolea kwa Mungu badala ya kuolewa, lakini mbele ya babu yake alikuwa hana uchaguzi; ilimlazimu kutii. Basi, vijana hao wakaamua kuishi kama ndugu badala ya kushirikiana kama mume na mke. Wakaishi hivyo muda wa miaka kumi na sita. Nyumba yao ikawa kimbilio la watu maskini wote waishio upande wao.

Pia wakawalea Yatima watatu na kuwafanya wana wao.

Maisha yao matakatifu na mazuri yaligeuka kabisa vita ilipolipuka kati ya Ufaransa na Uingereza.

Roberto akaenda akajiunga na jeshi.

Baadaye, akakamatwa vitani na fedha nyingi ilikuwa imedaiwa na Waingereza kabla ya kumwachilia. Yohana akauza lulu zake kwa ajili hiyo na Roberto akarudi kwao. Wakaishi vizuri sana tena mpaka mwaka 1362, Roberto alipofariki dunia.

Ndugu zake Roberto walimkasirikia Yohana kwa sababu alikuwa amewapa watu wengine sehemu kubwa ya mali yake na kwa hiyo wakamfukuza nyumbani mwake. Kwa umri alikuwa bado akubali kuolewa tena. Lakini akakataa, akakaa katika nyumba ndogo karibu na Kanisa, akajitolea kusali na kuwasaidia wagonjwa na watu maskini.

Alivumilia taabu nyingi, kama vile kuugua, kukosa vitu vya lazima na kuchukiwa na watu wenye kumwonea wivu.

Alilazimika kuomba-omba chakula na alifikiriwa na watu kama mwehu na mchawi.

Lakini baadaye, alipoanza kuzeeka, pole pole watu wakaanza kumtambua kama mtu Mtakatifu.

Wagonjwa waliponywa naye kimuujiza, aliwasaidia wengine waongoke kidini na alikuwa na kipaji cha ubashiri. Alikuwa na moyo wa huruma kwa wafungwa waliomo magerezani, hata kama walikuwa wahalifu wabaya. Aliwatembelea gerezani, aliwasaidia, aliwafundisha dini, na pengine alifaulu kuwaombea uhuru. Alifariki dunia mnamo mwaka 1414 na ibada yake ilikubaliwa na wakuu wa Kanisa mwaka 1871.

MWENYEHERI YOHANA MARIA MAYE, UTUOMBEE..

Post a Comment

أحدث أقدم