Ma
somo ya Misa 23/06/2024
Somo la Kwanza
Ayu 38:1,8-11
Bwana alimjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, Ni nani aliyeifunga bahari kwa milango, Hapo ilipofurika kana kwamba imetoka tumboni. Nilipolifanya wingu kuwa vazi lake, Na giza zito kuwa nguo ya kuifungia, Nikaiagiza amri yangu; Nikaiwekea makomeo na milango, Nikasema, Utafika mpaka hapa, lakini hutapita, Na hapa mawimbi yako yanyetayo yatazuiliwa?
Neno la Bwana, Tumshukuru Mungu
Wimbo wa Katikati
Zab 107:23-24, 25-26, 28-29,30-31(1b)
Washukao baharini katika merikebu,
Wafanyao kazi yao katika maji mengi,
Hao huziona kazi za Bwana,
Na maajabu yake vilindini.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Maana husema, akavumisha upepo wa dhoruba,
Ukayainua juu mawimbi yake.
Wapanda mbinguni, watelemka vilindini,
Nafsi yao yayeyuka kwa hali mbaya.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Wakamlilia Bwana katika dhiki zao,
Akawaponya na shida zao.
Huituliza dhoruba, ikawa shwari,
Mawimbi yake yakanyamaza.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametulia
Naye huwaleta mpaka bandari waliyoitamani.
Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake,
Na maajabu yake kwa wanadamu.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele.
Somo la Pili
2Kor 5:14-17
Upendo wa Kristo watubidisha; maana tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote; tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao. Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena. Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.
Neno la Bwana, Tumshukuru Mungu
Shangilio
Yn 14:6
Aleluya, aleluya
Mimi ndimi njia na ukweli na uzima asema Bwana: Mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi
Aleluya
Somo la Injili
Mk 4:35-41
Siku ile kulipokuwa jioni, Yesu akawambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna Imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?
Neno la Bwana, Sifa kwako Ee Kristu
إرسال تعليق