Kutukuka kwa Msalaba: Umuhimu wa Msalaba katika Maisha ya Mkristo
Sikukuu ya leo inaadhimisha uwakfu wa Basilika ya Kaburi la Yesu Kristo kule Yerusalemu. Kanisa hilo ni moja kati ya madhabahu maarufu sana duniani kwa sababu limejengwa juu ya mahali ambapo Bwana alisulubiwa na kuzikwa. Aidha, leo tunaadhimisha umuhimu wa Msalaba katika Maisha ya Kristo. Sisi wakristo tunautukuza Msalaba kwa sababu umebeba wokovu wetu, ndiye Kristo. Kutukuzwa kwa Msalaba kunahusishwa na uvumbuzi wa msalaba halisi aliosulubiwa Kristo uliofanywa na Mtakatifu Helena, mama wa Mfalme Konstantino, kwenye karne ya nne. Tofauti na tafsiri ya watu wengine, sisi kwetu Msalaba ni nguvu ya Mungu (1Kor 1:17-18). Tunapaswa kujivunia msalaba wa Kristo (Gal 6:14). Nayakati za mwanzo wakristo waliogopa kutumia Msalaba na kuonyesha hadharani. Sababu ya wapagani, wayahudi hata baadhi ya wakristo hawakuelewa inakuwaje Mungu asulubiwe Msalabani? Lakini pia waliogopa kujulikana kama wakristo wakati wa mateso kwa sababu Msalaba uliwatambulisha.
Ndugu wapendwa katika Kristo, leo Kanisa linaadhimisha Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba wa Bwana. Ni siku ya kutafakari tena juu ya fumbo la wokovu lililopatikana kupitia mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Msalaba, uliokuwa chombo cha aibu na laana, sasa umekuwa alama ya ushindi, wokovu na upendo usio na mipaka. Mtume Paulo anathibitisha wazi kuwa, “Kwa maana Kristo hakunituma kubatiza, bali kuhubiri Injili; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilishwa. Kwa maana neno la msalaba ni upuzi kwao wanaopotea; bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu” (1Kor 1:17-18).
Katika historia ya wokovu, Mungu aliwaonesha Waisraeli nguvu ya msalaba kwa mfano wa nyoka wa shaba. Walipokuwa njiani jangwani, walinung’unika na kuasi, na Mungu akawapelekea nyoka wenye sumu. Walipogeuka na kumwomba Musa awaombee, Mungu alimwagiza Musa kutengeneza nyoka wa shaba na kumuinua juu ya mti. Yeyote aliyemtazama aliokolewa (Hes. 21:4-9). Tukio hili linatufundisha kuwa wokovu unapatikana kwa kutazama kwa imani alama ya wokovu. Yesu mwenyewe anasema kuwa, “Kama vile Musa alivyomwinua nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa ili kila amwaminiye awe na uzima wa milele” (Yoh. 3:14-15).
Zaburi inatufundisha kwamba hata pale watu wa Mungu walipoasi mara kwa mara, Mungu alionyesha rehema na huruma. “Alipowaua, ndipo walipomtafuta; wakamrudia Mungu na kumtafuta kwa bidii. Wakakumbuka ya kuwa Mungu ndiye Mwamba wao, na Mungu Aliye juu ndiye Mkombozi wao. Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, wakamwambia uongo kwa ndimi zao. Moyo wao haukuwa thabiti kwake, wala hawakuwa waaminifu katika agano lake. Lakini yeye, kwa kuwa mwenye huruma, alisamehe uovu wao wala hakuwaharibu; naam, mara nyingi huigeuza hasira yake wala hakuamsha ghadhabu yake yote” (Zab. 78:34-38). Rehema hii ilithibitishwa kikamilifu pale Yesu alipokufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu.
Kwa hiyo, msalaba katika maisha ya Mkristo ni alama ya wokovu na kielelezo cha upendo wa Mungu. Paulo anasema, “Lakini mimi, hasha! Nisitukuze ila kwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo; kwa huo ulimwengu umesulubiwa kwa ajili yangu, nami kwa ajili ya ulimwengu” (Gal. 6:14). Hapa tunaona mtazamo mpya: msalaba si laana tena, bali ni chombo cha utukufu na utakatifu.
Katika maisha ya kila siku, Wakristo wanaitwa kuubeba msalaba wao kwa uaminifu na kumfuata Kristo. Msalaba unaweza kujidhihirisha katika mateso, changamoto, misalaba ya familia, maradhi, au magumu ya kijamii na kiroho. Hata hivyo, katika yote haya, tunakumbushwa kuwa msalaba si mwisho, bali ni daraja la kufikia utukufu wa ufufuko.
Leo tunaposherehekea sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba, tuangalie msalaba kama alama ya tumaini. Tukiwa na msalaba, hatupo peke yetu; Mungu yuko nasi. Tukijinyenyekeza mbele yake na kumkumbatia Kristo aliyesulubiwa, nasi pia tutashiriki utukufu wa ufufuko wake.
Tumsifu Yesu Kristo....
إرسال تعليق