MAISHA YA MTAKATIFU KAROLI BOROMEO, ASKOFU NOVEMBA 4
Karoli wa ukoo wa Boromeo alizaliwa mwaka 1538 karibu na mji wa Milano (Italia).
Alikuwa na akili nzuri, akajipatia digrii ya udaktari katika Sheria za Kiserikali na za Kanisa.
Mjomba wake Papa Pius wa Nne aliutambua utakatifu wa Karoli, akamweka kuwa Askofu wa Milano ingawa alikuwa kijana wa miaka ishirini na mitatu tu.
Askofu Karoli alifanya bidii kuyaeneza popote matangazo ya Mtaguso Mkuu wa Trent. Akajishughulisha sana kuondoa desturi mbaya zilizoingia katika Wakristo na Wamonaki na Mapadre wa Jimbo lake la Milano.
Yeye mwenyewe aliwatangulia kwa kuwaonesha mfano wake bora, alifuata mwenendo mgumu wa kitawa, kama vile angalikuwa mtawa.
Hakutaka kula nyama au samaki, wala kunywa divai. Alivaa shati lenye nywele na usiku alikesha akisali. Aliviuza vyombo vyote katika nyumba yake ili apate fedha za kujengea seminari.
Aliwaamuru Mapadre wa Jimbo lake wawafundishe Wakristo Katekisimu mara kwa mara, ili wote waijue vema dini, kwa maana wale ambao hawakuijua Katekisimu, hawakukawia kulegea katika dini.
Mwenyewe alifundisha dini kwa watu wa shamba na kwa watoto.
Lakini watu wabaya walimchukia.
Siku moja, muuaji aliingia kisirisiri Kanisani alimokuwa akisali Askofu Karoli pamoja na watu wa jumba lake, akataka kumpiga risasi, lakini risasi hazikumwumiza Askofu, bali zilianguka chini miguuni pake.
Wakristo wengi wa Milano waliyapuuza mashauri ya Askofu wao.
Hapo, walivyosema wakati ule, Mungu aliwaadhibu kwani watu wengi walikufa kwa ugonjwa wa tauni. Askofu Karoli akatoa amri yafanywe maandamano mjini na yeye mwenyewe alikuwako pia. Alichukua msalaba mkononi, akienda kwa miguu mitupu, akivaa kamba shingoni kama Askofu aliyestahili kunyongwa.
Hivyo ndivyo alivyoituliza hasira ya Mungu na watu wakapona.
Askofu Karoli Boromeo alitenda kazi nyingi sana, kwa sababu alikuwa mtu mwenye kupenda kusali na kufunga. Aliungama kila siku kabla ya kutoa sadaka ya Misa na aliposoma Breviari alipiga magoti kwa heshima.
Alikufa mwaka 1584, akatajwa Mtakatifu mwaka 1610.
MTAKATIFU KAROLI BOROMEO, UTUOMBEE..

Post a Comment