MAISHA YA WATAKATIFU ZAKARIA NA ELIZABETI, WAZAZI WA YOHANE MBATIZAJI
Zakaria na Elizabeti walikuwa wazazi wa Mtakatifu Yohane Mbatizaji.
Zakaria alikuwa kasisi wa Agano la Kale, naye Elizabeti mkewe alikuwa wa jamaa ya Haruni, Wote walikuwa wacha Mungu.
Walikuwa ni wenye haki mbele ya Mungu na waliendelea kuzishika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.
Walikuwa hawana mtoto, maana Elizabeti alikuwa tasa na wote wawili walikuwa wazee sana.
Basi, Zakaria alipokuwa katika zamu akifanya kazi za ukuhani hekaluni, Malaika alimtokea akamwambia: "Usiogope Zakaria, maana dua yako imesikilizwa na mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto mwanamume na jina lake utamwita Yohane.
Atakuwa mkuu mbele za Bwana; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye."
Mambo haya yakawa kama Malaika alivyosema. Elizabeti akamzalia Zakaria mtoto mwanamume, aliyeitwa Yohane, na sikukuu ya kuzaliwa kwake huadhimishwa 24 Juni.
Baada ya kuzaliwa Yohane, hatusikii habari zaidi za Zakaria na Elizabeti.
Sikukuu yao inaadhimishwa sana katika Makanisa ya Mashariki na imeenea pia katika Makanisa popote ulimwenguni.
WATAKATIFU ZAKARIA NA ELIZABETI, MTUOMBEE..

Post a Comment